WAZIRI MKUU AGEUKA MBOGO KWA WATUMISHI WA UMMA WATAKAO JIMILIKISHA VIZIMBA VYA SOKO JIJI LA ARUSHA ASISITIZA KUWAFUTA KAZI.
🔺️ARIDHISWA NA MIRADI YA MAENDELEO, ATAKA MIKAKATI IKAMILIKE HARAKA YA MABASI YA MWENDO KASI JIJI LA ARUSHA.
Na Lucas Myovela - Arusha.
"TAHADHARI Sitarajii vibanda hivi vichukuliwe na watu wasiyofanya biashara na baada ya hapo wao wawapangishie wanaofanya biashara, Hii haitaji mtu wa kati, Ulanguzi, Unyonyaji na wizi, Sasa Mkurugenzi hatutarajii watumishi wa jiji hawafanyi biashara humo na tuwakute wao ndiyo wanashikilia vibanda, Hapa hakuna cha kushika eneo ambalo wewe haufanyii kazi.
Na kama kuna eneo lolote mfanyabiashara ukagundua eneo unalofanyia kazi kuna mtu wa kati na hata akiwa ni mtumishi wa umma atakuwa amesha poteza kazi yake, ridhikeni na mishara yenu mnayo ipata haya masoko waachieni wananchi na hili hasa ndilo analolitaka Rais Dkt. Samia wananchi hawa wainuke kiuchumi.
Nimeona matoleo hapa panatakiwa kuwa na BRT sasa kwa viwango ambavyo vimeshafanyika kwenye majiji mengine ambayo ni wenyeji wa AFCON na sisi hapa twende kwenye viwango hivyo hivyo tuwe na magari ya mwendo kasi tena hasa yenyekutumia nishati safi. Nimelidhishwa na hatua ujenzi wa stendi ilipofika ila inatakiwa kwa muda uliyobaki tukimbize mradi huu ili kufidia muda ambao tumechelewa".
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, ameridhishwa na kasi pamoja na ubora wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo jijini Arusha.
Miradi hiyo ni ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Bondeni City Bus Terminal na Soko la Kilombero, ambapo ameeleza kuwa ameona thamani ya fedha na usimamizi imara na akisisitiza uwajibikaji, matumizi sahihi ya fedha za umma na uboreshaji wa mazingira ya biashara kwa wananchi wa Jiji la Arusha.
Ameyasema hayo leo Februari 24, 2026 wakizungumza wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Soko la Kilombero Jiji Arusha, Amnmbapo ameeleza kuwa kukamilika kwa stendi mpya ya mabasi inayojengwa katika kata ya Murieth kutapunguza msongamano uliopo sasa, kupanua huduma za usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika jiji hilo.
"Stendi ya sasa ni finyu na imebana sana, Mradi huu mpya utaongeza nafasi kuboresha huduma na kufungua fursa zaidi za kibiashara kwa wananchi," Amesema Dkt. Mwigulu.
Katika kuimarisha miundombinu ya jiji, Dkt. Nchemba alielekeza baadhi ya barabara muhimu zijengwe kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa mijini.
Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo, kuongeza idadi ya masoko rasmi ili kuwapa wafanyabiashara maeneo bora, salama na yenye wateja wa uhakika.
Alisisitiza kuwa soko jipya la Kilombero litawapa kipaumbele wafanyabiashara waliopisha eneo la mradi huo, huku akionya vikali vitendo vya ulanguzi, wizi na upendeleo katika ugawaji wa maduka.
"Nataka haki itendeke, Fanyeni sensa kubaini wahusika halali. Mtumishi wa umma atakayebainika kujimilikisha duka kinyume cha utaratibu atachukuliwa hatua kali". Amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, alielekeza masoko yote yawe safi salama na yaendeshwe kwa mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu, kudhibiti udanganyifu na kulinda mali za wafanyabiashara.
FAIDA YA MIRADI HII YA KIMKAKATI.
Miradi ya Kimkakati ya Jiji Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi wa Jiji alisema ziara ya Waziri Mkuu ni motisha kwa wafanyabiashara na jamii kwa ujumla, ikionyesha dhamira ya serikali kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi.
Kituo cha Mabasi cha Bondeni City kinajengwa kwa miundombinu ya kisasa ikiwemo maegesho ya magari makubwa na madogo, maeneo ya kupakia na kushusha abiria, mifumo ya usalama na huduma za mizigo.
"Ujenzi wa Kituo Kikuu Cha Mabasi (Bondeni City Bus Terminal), unatekelezwa katika eneo la mita za mraba 129,671 lililopo eneo la Bondeni City, Halmashauri ya Jiji la Arusha.Ikiwa na jumla ya eneo litakalojengwa miundombinu yote ni mita za mraba 11,185 ikiwemo Kituo cha kupokelea na kushusha abiria, uboreshaji wa Mazingira na ujenzi wa barabara ya kuingia ndani ya kituo". Amesema Kayombo.
"Utekelezaji wa ujenzi wa Kituo Kikuu Cha Mabasi Arusha unatekelezwa na kampuni ya M/S MOHAMMEDI BUILDERS LIMITED, kampuni ya mtanzania mzawa, yenye makao makuu yake Jijini Dar Es Salaam Tanzania, kwa gharama ya Shilingi Bilioni 14.317. na unasimamiwa na Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Mhandisi Consultancy Ltd kwa ushirikiano na kampuni ya GBS Consultant Ltd". Ameongeza Kayombo.
Aidha Kayombo ameeleza kuwa Mradi huo ni mojawapo ya miradi minne inayotekelezwa na Jiji la Arusha chini ya mradi wa TACTIC kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) ambayo ni Ujenzi wa Soko la Kilombero, Ujenzi wa Soko katika eneo la Mrombo, na Ujenzi wa Bustani ya Mapumziko (Themi Living Garden) iliyopo ndani ya Jiji la Arusha eneo la Themi.
Mradi unahusisha uboreshaji wa mazingira, mifumo ya maji ya mvua na maji taka, maegesho ya magari na miundombinu rafiki kwa watu wote, wakiwemo wenye uhitaji maalum.
Akitoa taarifa juu ya Mradi wa soko la Kilombero Mkurugenzi John Kayombo, ameeleza kuwa Soko hilo limepangwa kwa viwango vya kisasa likiwa na Vizimba 518 vinavyoweza kuhudumia wafanyabiashara 2,072 kwa wakati mmoja,Maliwato ya kisasa kwa jinsia zote na kwa wazee na wenye uhitaji maalum ( walemavu).
Pia soko hilo lina Kituo cha polisi, ofisi ya zimamoto na chumba cha huduma ya kwanza Bustani ya mapumziko na maegesho rasmi ya magari, malori, boda boda na bajaji
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Mohammedi Builders Limited kwa gharama ya Shilingi bilioni 9.5. Ulianza Mei 30, 2025 na unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2026.
Hadi sasa mradi umefikia asilimia 66 ya utekelezaji, huku mkandarasi akilipwa Shilingi bilioni 3.95 sawa na asilimia 41.66 ya gharama ya mradi.
Mradi wa soko unatarajiwa kuongeza ajira, mapato ya wafanyabiashara na mapato ya Halmashauri ya Jiji la Arusha. Pia utaimarisha huduma za kifedha, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji kwa kuwepo maegesho ya vyombo vya usafiri.
Pia utaimarisha huduma za kifedha, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji kwa kuwepo maegesho rasmi ya vyombo vya usafiri.
Pamoja na changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya vifaa wakati wa uchaguzi mkuu iliyosababisha ucheleweshaji wa asilimia 5.5, mkandarasi ameongeza zamu za usiku ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Halmashauri ya Jiji la Arusha imetoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo, pamoja na ziara ya Waziri Mkuu iliyolenga kuimarisha usimamizi na kasi ya maendeleo.
Comments
Post a Comment