BODI YA MIKOPO YATETA NA WATENDAJI WA KATA.


Na Lucas Myovela_ Arusha

Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Nchini imekutana na watendaji wa kata 158 kutoka Wilaya 7 za Mkoa wa Arusha kwa ajili la kuweka mkakati wa kuwatambua wanufaika wa mikopo iliyotolewa na Bodi hiyo.

Akizungumza katika kikao kazi cha mikakati ya kutengeneza mfumo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Abdurazak Badru amesema kupitia kundi hilo wataweza kulifikia kundi kubwa la wanufaika wa mikopo ili waweze kutambua mikopo yao na waweze kuanza kuirejesha.


Aidha amesema kuwa katika tafiti walizozifanya waligundua urejeshaji wa mikopo kuchukuwa muda mrefu, hivyo mkakati huo utawasaidia kuwafikia wale ambao hawajajipanga kurejesha mipoko hiyo.


Ameongeza kuwa kikao hicho ni moja kati ya muendelezo wa kampeni ya Sifurisha ambayo inampa mnufaika wa mkopo unafuu wa kurejesha kwa wakati mmoja ambapo takribani wanufaika zaidi ya laki tano wameweza kukopeshwa mkopo huo.


"Tumeanza na mkoa wa Arusha maana ni mahususi kwasababu una shughuli nyingi za kiuzalishaji za biashara,utalii pamoja na kilimo na baadae kwa kutumia uzoefu wa Mkoa wa Arusha tutakwenda kwenye mikoa mingine."


Sambamba na hayo amesema kwa sasa wameboresha mazingira ya urejeshaji wa mikopo kupitia mtandao na tayari utaratibu wa kumuwezesha muajiri kuweza kukata na kurejesha mkopo wa mnufaika zimekamilika  kupitia kipengele cha Lipa kwa mnufaika na kipengele cha Ipo kwa mwajiri kinachompa fursa ya kuweka taatifa, kukata na kurejesha bila kusafiri kwenda katika ofisi zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akifungua kikao hicho amesema hatua hiyo ambayo inafanywa na Bodi ya Mikopo ni jambo ambalo linapaswa kuungwa mkono kqani mfumo unaotumika umesaidia kuongezeka kwa wanufaika.


Hata hivyo Mongela amewaagiza wote kuwajibika kwa kuwahamasisha wanufaika hao ili waweze kurejesha mikopo yao kwa hiyari ambapo amesema Mkoa wa Arusha utakuwa wa mfano na ofisi yake itasimamia zoezi la kuhakikisha azimio la kikao hicho linafanikiwa.


Ameongeza kuwa fedha zinayotolewa ni fedha za umma hivyo Mkoa wa Arusha ukichangia katika urejeshaji utakuwa umefanya jukumu lake na wajibu wake katika kuimarisha uzalendo.


"Fedha hizi za mikopo zikirudi Bodi ya mikopo inazidi kujijengea uwezo,mwisho wa siku vijana wetu na watoto wetu wengi zaidi watapata elimu na uwezo  wao wa kuchangia kwenye maendeleo utakuwa mkubwa zaidi kuliko ulivyo sasa."Alisisitiza Jonn Mongela Mkuu wa Mkoa wa Arusha

Vilevile amesema kwa dhana ya Sifurisha na ya kukata shauri itasaidia nchi kurudisha mikopo ambayo imetolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Comments