DKT, TULIA; CRDB MFANO WA KUIGWA KWA TAASISI FEDHA HAPA NCHINI.

Na Lucas Myovela_ Arusha.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson amesema ukuaji mkubwa wa faida uliopata benki ya CRDB unastahili kuwa mfano wa kuigwa na taasisi zingine za fedha nchini.

Dkt Tulia ametoa pongezi hizo leo jijini Arusha wakati akifungua semina ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa wake na Watanzania kwa ujumla wakati wakijiandaa na Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa unaofanyika Mei 22 mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha AICC.

Amesema ukuaji huo umetokana na uwekezaji na usimamizi mzuri katika uendeshaji wa benki hiyo hivyo, kuwawezesha wanahisa kupata gawio ambalo sasa litaongezeka hadi kufikia asilimia 64 kwa hisa.


Dkt Tulia amesema benki hiyo imeendelea kudhihirisha kwa vitendo kuwa Benki kiongozi nchini kwani kila mwaka imekuwa ikitengeneza faida ya uwekezaji kwa wanahisa wake na kuzitaka taasisi nyingine za umma na binafsi kuiga mfano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi benki hiyo, Dkt Ally Laay amesema wanajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa.


 “Niwakaribishe Watanzania wengine waje kuwekeza ndani ya Benki yetu ili nawao waanze kunufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na Benki yao,” aliongezea Dkt. Laay.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo Wanahisa wao pamoja na Watanzania wengine ili kuwajengea uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hususan katika soko la hisa la Da es Salaam.


“Kwa kutoa elimu hii Wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika Benki yao ya CRDB, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha na Watanzania wengine pia kuwekeza katika hisa hususan za Benki ya CRDB na kuanza kupata gawio,” aliongezea Nsekela.

Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha Wanahisa katika Mkutano Mkuu utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kupitia Mtandao. “Mkutano utaanza saa 3 asubuhi, watu wa mtandaoni wataweza kujiunga kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App,” alisema Nsekela.

Benki ya CRDB imeweka muongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yake ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii ya Instagram, twitter, lakini pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa Wanahisa.



Comments