MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA USAHIHISHAJI MITIHANI WAPUNGUZA MALALAMIKO.

Posted by; Lucas Myovela.
DAR ES SALAAM.

Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imepongeza Wizara ya Elimu na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa kuwa na mfumo wa kielektroniki wa usahihishaji mitihani ambao umerahisisha zoezi la usahihishaji mitihani ya Taifa.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo wakati Kamati ilipofanya ziara katika Taasisi hiyo ambapo mfumo huo kwa sasa unatumika kusahihisha mitihani ya darasa la Saba na Ualimu.

Kamati hiyo pia imeishauri Wizara kuwatambua kitaifa Watanzania waliovumbua mfumo huo kutokana na kuwa umejibu changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kufupisha muda wa usahihishaji.

"Huu uvumbuzi unatakiwa ulindwe na muone namna bora ya kuwatambua Kitaifa wavumbuzi wa mfumo huu pamoja na kuubiasharisha kwani Watanzania wengi wana imani kubwa na utendaji kazi wake uliofanikiwa kupunguza malalamiko kwa kiasi kikubwa," amesema Mhe. Nyongo.

Kamati hiyo imetoa maoni na mapendekezo ya kuimarisha utendaji ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kutosha vitakavyowezesha mfumo huo kutumika Kikanda ili kurahisisha zaidi zoezi la usahihishaji mitihani.

Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga (Mb) ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea NECTA na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NECTA, Prof. William Anangisye amesema kuwa kwa sasa wataalamu wanaendelea kuandaa mifumo kwa ajili ya usahihishaji wa mitihani ya Darasa la Nne na ile ya Sekondari.





Comments