VYUO VYOTE NCHINI VYATAKIWA KUFANYA _TRACER STUDY_ KWA WAHITIMU.

VYUO VYOTE NCHINI VYATAKIWA KUFANYA _TRACER STUDY_ KWA WAHITIMU ILI KUSAIDIA WAAJIRI KUJUA UTENDAJI KAZI NA UMAHILI WA MUHITIMU.

Na WyEST, DAR ES SALAAM.

Wito umetolewa kwa Vyuo vyote nchini kufanya _tracer study_ ya wahitimu kutoka katika vyuo vyao ili kupata mrejesho wa waajiri kuhusu utendaji kazi na umahiri wa wahitimu.


Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph ambapo amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kupata tathmini juu ya elimu inayotolewa katika vyuo hapa nchini.

"Kila chuo kinajua kinafundisha vizuri na wanafunzi wake wanafanya vizuri lakini _tracer study_ itatusaidia kujua kutoka kwa waajiri iwapo wahitimu wana viwango wanavyotaka au la, na pia kutoka kwa mhitimu kujua iwapo elimu aliyopata inamsaidia katika utendaji kazi wake," amefafanua Prof. Mkenda 


Aidha Waziri Mkenda amevihakikishia vyuo vyote binafsi kuwa juhudi za mageuzi ya elimu na utekelezaji wa Sera ya Elimu utafanywa kwa kushirikisha umma na sekta binafsi kwa kuwa linahusu wote na ni la kudumu.

"Iwapo mna maoni au mapendekezo ambayo mngependa Serikali iyasikie tunawakaribisha na kuwahakikishia kuwa milango yetu iko wazi wakati wote hata baada ya mapitio ya Sera kupita," amesema Prof. Mkenda.


Mkenda ameongeza kuwa msukumo wa Serikali ni kuendelea kuongeza fursa za elimu ya juu ambapo amesema Wizara inajenga kampasi mpya 14 za vyuo vikuu, na kusisitiza juu ya kusimamia suala la ubora wa elimu.

"Pamoja na kuongeza vyuo hatutaacha kusimamia suala la ubora" amesema Mkenda

Awali Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Elias Opiyo amesema idadi ya wahitimu imeongezeka kwa asilimia 48.1 kutoka 416 na kufikia 616 ambao kati yao wanaume ni 421 na wanawake ni 195 hatua ambayo chuo kinajivunia.


Ameongeza kuwa tayari chuo kimehuisha mitaala yote ya Shahada za Kwanza na Stashahada, pia kinaandaa mitaala mipya ili kukidhi mahitaji ya kitaalamu na kitaaluma ya sasa na ya baadae.

"Chuo chetu kinatekeleza miradi ya kitafiti ikiwa ni pamoja na miradi iliyo kwenye maeneo ibuka ya kisayansi na kiteknolojia kama vile akili bandai (artificial intelligence), mtandao wa vitu (internet of things), mashine kujifunza (machine learning) na teknolojia ya satelaiti (satellite technology)," amesema.


Jumla ya wahitimu 616 wametunukiwa Stashahada na Shahada za Kwanza katika fani mbalimbali za Uhandisi, Udaktari, Ufamasia, Ukunga na Ualimu wa sayansi na hisabati.

Comments