MILIONI 470 ZA MRADI WA SEQUIP WAKAMILISHA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI LENJULU

Na Mwandishi wetu _ Dodoma.

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius J. Ndejembi ameipongeza halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa kusimamia kikamilifu fedha za ujenzi wa shule mpya ya Kata ya Lenjulu ambayo majengo yote yamekamilika na wanafunzi wanaendelea na Masomo.


Ameyasema hayo leo tarehe 25 Aprili 2023 wakati akikagua ujenzi wa shule shule mpya ya Lenjulu katika wilaya Kongwa mkoani Dodoma uliogharimu shilingi milioni 470 kupitia Mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

“Napongeza uongozi wa Wilaya Kongwa kwa Usimamizi mzuri wa shilingi Milioni 470 iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga shule hii mpya na kuhakikisha inakamilika, Sisi tunachukua mfano huu mzuri wa shule ya Lenjulu ili tuweze kupeleka na maeneo mengine” amesema Ndejembi


Ndejembi amesema Wilaya ya Kongwa ni moja ya Halmashauri iliyosimamia vizuri ujenzi wa shule hizo zilizojengwa katika Halmashauri zote nchini na imehakikisha majengo yote yanakamilika ikiwa ni pamoja na Maabara zote tatu na chumba cha TEHAMA.


Aidha, Ndejembi amewataka wazazi na wananchi wa kata ya Lenjulu kuhakiksha wanafunzi wanafika shule na kuondokana na utoro na mdondoko wa wanafunzi shuleni pamoja na kutunza miundombinu ambayo Serikali imejenga ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu ya Sekondari katika maeneo ya karibu.


Pia amewakikishia kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI itahakikisha inaongeza Walimu kupitia Kibali cha ajira mpya 21,200 kilichotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi huu, ambapo nafasi za kada ya Ualimu ni 13,130.


Ndejembi amemuagiza Mkurugenzi Halmashauri ya Kongwa kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu na kuhakikisha maji yanafikishwa katika shule hiyo ili wanafunzi wasipate adha ya Kwenda kuchota maji mbali na maeneo ya shule.


Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Mradi wa kuboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ilitoa shilingi milioni 470 ya Ujenzi wa shule mpya ya Kata kwa kila Halmashauri kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 8, jengo la utawala 1, maabara 3, maktaba 1, chumba cha TEHAMA 1, matundu ya vyoo 20 (wasichana 10 na wavulana 10), ununuzi wa tenki la maji 1, ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji na kunawa mikono.


Comments