PROF. SEDOYEKA AMALIZA UTATA JUU YA TUHUMA ZILIZO MKABILI KAMATI YA MAADILI.

🔴ATOA MSIMAMO WAKE WA KUILINDA NCHI KAMA KIONGOZI MWADILIFU KWA MASLAHI MAPANA YA MAENDELEO YA TAIFA.


🔴ATUMIA ZAIDI YA MASAA MATATU KUTOA UTETEZI WAKE MBELE YA BARAZA LA MAADILI KATIKA TUHUMA 4 ZILIZOKUWA ZIKIMKABILI.

By Lucas Myovela.

Baada ya Baraza la Maadili kuanza kusikiliza malalamiko dhidi ya tuhuma zinazomkabili Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka hapo jana Oktoba 16,2024, kwa matumizi mabaya ya ofisi, kinyume na kanuni na taratibu za maadili ya uongozi wa umma, tuhuma hizo zilizo wasilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali.

Akitoa utetezi huo leo Oktoba 17,2024 kwenye kikao cha baraza hilo jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Baraza hilo Jaji Mstaafu Rose Teemba na upande wa mlalamikaji uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Emma Gellan na Hassan Mayunga, ambapo Prof. Sedoyeka amekana kutokuhusika kwa chochote na kuweka msimamo wake wa uadilifu uliyo tukuka mbele ya taifa lake.


Akijibu tuhuma hizo Prof. Sedoyeka, ameeleza kuwa katika tuhuma ya kwanza ya kuwa karibu na Bw. Hakimu Ndatama na uhamisho wake kurudi IAA.


"Pindi mimi niliporejea kuwa Mkuu wa Chuo Uhamisho wa Bw. Ndatama kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii ulifuata taratibu zote za kisheria na kufuatia mahitaji ya kikazi, Chuo kiliandika barua kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuomba Bw. Ndatama arejeshwe". Amesema Prof. Sedoyeka.


"Hili la kuomba arejeshwe lilifanyika kabla hata ya mimi kurejea  tena katika Chuo cha IAA kutokana na mahitaji ya kikazi dhidi ya waajiri wangu". Aliongeza Prof. Sedoyeka.


"Mimi niliripoti Machi 13, 2023 niliporudishwa IAA lakini barua ya Hakimu kuomba kutoka Wizara ya Maliasili na kurudishwa IAA ilitolewa Machi 9, 2023,". Alisisitiza Sodoyeka.


Katika tuhuma ya pili iliyokuwa ikimkabili Prof. Sedoyeka ni kufanya uteuzi na kumpandisha cheo Bw. Hakimu Ndatama kutoka Afisa Rasilimali kuwa Mkuu wa sehemu ya rasilimali watu, kabla ya kukamilika kwa uhamisho wa mtumishi huyo pasipo kuwa na sifa.


"Kuhusu tuhuma ya kutekeleza uteuzi wa Bw. Hakimu Ndatama na mgongano wa maslahi, napenda kueleza baraza hili  kuwa uteuzi huu ulikuwa na msingi mzuri unaozingatia uwezo na ufanisi wake katika utekelezaji wa majukumu yake, Nilizingatia sifa za Bw. Ndatama na uwezo wake wa kuchangia maendeleo ndani chuo cha IAA". Amesema Prof. Sedoyeka.


"Nikiwa na dhamira ya kulinda maslahi ya taasisi na kuhakikisha tunapata watu wenye uwezo wa kuchangia katika malengo yetu ya taasisi, Bw. Ndatama si ndugu yangu, si kabila langu, si dini yangu, si rafiki yangu na wala hakuna chochote kinachoniunganisha naye, Sina maslahi naye kwa namna yoyote sasa ningeweza kufanya hivyo ila nilizingatia ubora wake wa kiutendaji ili tuweze kupiga hatua kama taasisi". Aliongeza Prof. Sedoeka.


Aidha katika shitaka la tatu lililokuwa likimkabili Prof. Sedoyeka ni kuingilia mchakato wa zabuni ya ununuzina ufungaji wa viti na meza katika kampasi ya Babati kwa kuifuta bila kufuata utaratibu na bila sababu za kisheria ziliainishwa, chini ya kifungu cha 59 2 cha sheria ya ununuzi wa umma sura ya 410.


"Kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, Na. 7 ya mwaka 2013), inampa mamlaka Afisa Masuuli kukataa kuendelea na zabuni ama kurejesha zabuni kwenye Bodi ya Zabuni, vifungu hivyo vimefafanua kwamba atakapofanya hivyo ataeleza sababu na kupata idhini ya Bodi ya zabuni (Tender Board)". Amesema Prof. Sedoyeka.


"Ninaweka wazi msimamo wangu kwamba nilifuata taratibu zote na sikuvunja sheria bali nilikuwa nikitekeleza majukumu yangu kwa mujibu wa Sheria, kama kiongozi mwaminifu kwa nchi yangu, nimekuwa makini kuhakikisha taasisi inapata bidhaa bora kwa njia za uwazi na kwa gharama nafuu kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma". Alionheza Prof. Sedoyeka.


"Katika mazingira yote ya manunuzi ya umma, dhamira yangu kama Afisa Masuuli ni kuongeza wigo wa ushindani kwa lengo la kupata thamani halisi ya pesa za Umma (value for money). Hivyo nimekuwa na msimamo wa uwazi na kuzingatia taratibu zinazotakiwa, kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa na kuimarisha taasisi ili iweze kufikia malengo yake ya kutoa elimu bora kwa jamii". Amesisitiza Prof. Sedoyeka.


Amesema katika zabuni hiyo kuna wazabuni ambao walitoa bei nafuu kuliko ambaye alikuwa amepitisha ambaye ni kampuni ya Jaffer na bei yake kwa kiti na meza ni Sh. 440,000 huku Timber ilikuwa Sh.389,000 na Vadeck ni Sh.346,000.


"Nilipokuta mwenye gharama kubwa ameshinda ndipo nikafuatilia mchakato wa hii zabuni, nilibaini viliwekwa vigezo maalum vya bidhaa hiyo na maelezo ya tathmini iliyofanywa na kamati ya manunuzi ilifafanua kwenye bidhaa ya kampuni moja huku kukiwa hakuna maelezo ya kampuni zingine". Amesem Prof. Sedoyeka.


Pia ktika shitaka la nne lililokuwa likimkabili Prof. Sedoyeka ni kwamba mlalamikiwa wakati akitekeleza majukumu yake ya uongozi wa umma, alifanya uhamisho wa ndani wa mtumishi Bw. Robert Mwitango Afisa Ugavi kutoka kitengo cha ununuzi na ugavi kwenda idara ya maktaba tofauti na sifa za kitaaluma za mtumishi huyo.


"Kwa ujumla uhamisho wa ndani wa watumishi hufanywa kwa lengo la kuboresha ufanisi wa kiutendaji wa taasisi husika". Amesema Prof. Sedoyeka.


"Katika Mwaka wa 2023/2024 Idara ya Maktaba ilipanga kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo zile ambazo kwa uhalisia wake zilihitaji msaada wa karibu wa kitengo cha Manunuzi ya Umma, kama Stock taking, Asset Verification” na Ununuzi mkubwa wa vitabu kwa mkupuo". Aliongeza Prof. Sedoyeka.


"Nilipotathmini ukubwa wa majukumu hayo, unyeti wake na namna yanavyohitaji utaalamu wa manunuzi ya umma, niliamua mtumishi mmoja afanyiwe uhamisho wa ndani kutoka kitengo cha Manunuzi kwenda Idara ya Maktaba". Amefafanua Prof. Sedoyeka.


Aidha, ameomba baraza hilo lisimtie hatiani kwenye tuhuma hizo na kwamba anafanya kazi kwa hali na nguvu ili kuleta mafanikio kwenye taasisi hiyo na hakuwa na nia ovu na ataendelea kuitumikia IAA.


Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Teemba amesema wamepokea ushahidi wa pande zote mbili na baraza limekamilisha kazi yake na baada ya uchambuzi litawasilisha taarifa yake sehemu husika.

Comments