DKT. MPANGO AITAKA BENKI KUU NA BENKI ZILIZO CHINI YA TBA KUPITIA KANUNI NA SHERIA ZINAZO SIMAMIA SEKTA YA FEDHA ILI KUEPUKA UPOTEVU WA RASILIMALI
🔻AWAPONGEZA CRDB KWA KUENDELEA KUREJESHA KWA JAMII NA KUTANUA WIGO KATIKA SEKTA YA FEDHA.
Na Lucas Myovela -Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Benki Kuu pamoja na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kupitia sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya fedha kimataifa na kiinchi ili kulinda na kuepuka hatari ya kupoteza rasilimali.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa Benki ya CRDB kuweka mkazo zaidi katika udhibiti wa tishio la uhalifu wa kimtandao ili kujenga imani ya wateja na kulinda heshima ya benki hiyo. Amesema Benki ya CRDB haina budi kujihami mapema na wakati wowote kwa sababu, kukua kwa matumizi ya teknolojia kumeleta wimbi la matukio ya uhalifu wa kimtandao unaohatarisha mitaji ya benki duniani na kuongeza gharama za kukabiliana nao.

Katika kulinda mazingira, Makamu wa Rais ametoa rai kwa mabenki kuangalia uwezekano wa kuunganisha nguvu kwa kuwa na miradi ya pamoja na Taasisi nyingine za fedha, ili kupata kiwango kikubwa zaidi cha fedha na kuziba pengo la ufadhili wa miradi ya mazingira ambalo bado ni kubwa mno.
Makamu wa Rais amesema Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa sekta ya fedha inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi. Amesema Serikali imeboresha sera na kuweka mifumo madhubuti, imejenga miundombinu wezesha na imeendelea kukuza uchumi wa nchi na kipato cha wananchi.
Ameongeza kwamba, Serikali ilipitisha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ili kuweka msingi imara wa kisheria kwa uendeshaji wa benki na taasisi nyingine za kifedha nchini. Kadhalika, Serikali imetengeneza sera mbalimbali zikiwemo, Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2000, Mpango wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (Awamu ya Kwanza 2014-2016, Awamu ya Pili 2018-2022 na Awamu ya Tatu 2023-2028), Mpango wa Taifa wa Elimu ya Fedha (2016-2020), Programu ya Kutoa Elimu ya Fedha kwa Umma (2021/22 – 2025/26), Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017, Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (2020/21 -2029/30) pamoja na Sheria ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imepokea kwa furaha ujenzi wa shule ya sekondari ya mfano itakayojengwa na Benki ya CRDB katika Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam ambayo pamoja na ubora wa miundombinu ya ufundishaji inayotarajiwa kuwa dira kwa shule zingine za umma na binafsi. Amesema zawadi hiyo ni ya kipekee kutoka kwa benki kwenda kwa jamii.
Prof. Mkenda ameihakikishia Benki ya CRDB kwamba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kushirikiana kwa karibu na benki hiyo kwa maslahi ya Taifa na kwa maendeleo ya Elimu kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Dkt. Laay amesema Benki ya CRDB itaendelea kuwa mshiriki namba moja wa maendeleo kwa Serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wateja wote.

Nsekela amesema Benki hiyo inajivunia kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa sera za mazingira, jamii na utawala bora. Amesema mwaka 2019 ilikuwa Benki ya kwanza Afrika mashariki na kati kusahiliwa na shirika kubwa duniani la mazingira la GCF na kupewa daraja la kati kusimamia miradi yenye kiwango cha zaidi ya dola milioni 200.
Comments
Post a Comment