WAFANYAKAZI WA RADIO FREE AFRICA (RFA), WATOA ZAWADI ZA KRIMASI NA MWAKA MPYA KWA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM BUHANGIJA.

 Wafanyakazi wa Kituo cha Matangazo Radio Free Africa (R.F.A)  wamesherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya 2022 kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi ( ualbino), viziwi na watu wasioona wanaolelewa katika kituo cha Buhangija Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo Kiongozi wa msafara wa wafanyakazi wa Radio Free Africa (RFA) waliofika katika kituo cha Buhangija Jumatano Desemba 2021, Yusuph Magasha amesema wameamua kusherehekea Sikukuu za mwisho wa mwaka 2021 na kufungua mwaka 2022 kwa kutoa zawadi kwa watoto hao.
“Kwa niaba ya wafanyakazi wa Radio Free Africa,mimi na msafara huu tumekuja kukabidhi zawadi hizi ambazo tumechangishana sisi wafanyakazi wa Radio Free Africa pamoja na wadau wetu ili watoto wetu wafurahie sikukuu hizi za mwisho wa mwaka 2021 pamoja na kufungua vizuri mwaka mpya 2022”,ameeleza Magasha.

Amezitaja miongoni mwa zawadi hizo ni pamoja na Taulo za Kike ‘Pedi’, mchele,unga wa sembe, mafuta ya kupikia,maharage,sukari mafuta ya kujipaka, sabuni, dawa za meno,majani ya chai,madaftari,kalamu,juisi,pipi na biskuti.
“Naomba mpokee hiki kidogo ambacho tumewaleteeni na tunaahidi kuendelea kuja hapa Buhangija ili kuwatelea mahitaji mbalimbali”,amesema.

Magasha ametumia fursa hiyo kuwaasa watoto hao kuzingatia masomo yao akiwasisitiza kuwa elimu ndiyo kila kitu katika maisha yao.
Akiwa katika kituo hicho mmoja wa watangazaji wa Radio Free Africa, Wambura Mtani ameahidi kuwa atakuwa anampatia mahitaji mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho cha Buhangija.

Kwa upande, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Msingi Buhangija Loyce Daudi amewashukuru wafanyakazi wa Radio Free Africa kutembelea kituo cha Buhangija na kuwapatia mahitaji mbalimbali huku akizitaja baadhi ya changamoto zilizopo kuwa ni Bili kubwa za maji zinazotokana na miundo mbinu chakavu ya maji pamoja na uhaba wa vifaa vya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi hao.
Nao watoto wameeleza kufurahia ugeni wa waandishi wa habari na watangazaji wa Radio Free Africa, kuzungumza Mbashara 'Live' kupitia RFA na kuwashukuru kwa kuwapatia zawadi za Krismasi na Mwaka Mpya yakiwemo mahitaji ya vifaa vya shule yakiwemo madaftari na kalamu.

Miongoni mwa waandishi wa habari na watangazaji wa Radio Free Africa waliotembelea kituo cha Buhangija ni Wambura Mtani, Debora Mpagama, Emmanuel Mkuwi,Froza Mhando,Renatus Kiluvia, Pauline David, Nassoro Dimoso, Yusuph Magasha na dereva wao Andrew John.

Comments

Post a Comment