RTO ARUSHA; MADEREVA WA SERIKALI MJITATHIMINI.

 Na Lucas Myovela_ Arusha.


Jeshi la polisi Mkoa wa Arusha, limewaonya vikali madereva wa serikali ambao wamekuwa chanzo cha kusababisha  ajali za usalama barabarani na kuapa kuwashughulikia kama wahalifu wengine bila kujali anayemwendesha anawadhifa gani.

Aidha madereva hao wametakiwa kuacha kutumia kimvuli cha viongozi kuvunja Sheria badala yake wake chanzo Cha kutoa ushauri kwa kiongozi anayelazimisha  mwendo kasi.

Akifungua mkutano mkuu ulioambatana na mafunzo kwa madereva hao mkoani Arusha,mkuu wa kikosi cha usalama barabarani (RTO) Mkoa wa Arusha, Solomon Mwangamilo alisema kuwa kumekuwepo na wimbi la ajali zinazotokana na uzembe wa madereva wa serikali na kuagiza Askari wa usalama barabarani kutowafumbia macho.

Akizungumza na madereva wa serikali zaidi ya 200 kutoka mikoa mbalimbali nchini ,Mwangamilo aliwakumbusha wajibu wa madereva hao katika kusimamia Sheria na kuwataka wasijione wapo juu ya Sheria kwani Sheria ni msumeno na watashughulikiwa kama wahalifu wengine wanaovunja Sheria .

"Nataka wawe mfano kwa madereva wengine ,wabadilike kifikira, kimawazo na kivitendo wajibu wa jeshi la polisi ni kusimamia Sheria na hatutasita kuchukua hatua Kali dhidi yao kwani hawapo juu ya sheria"alisema.

Alisema kuwa Madereva hao wanaposhindwa kutii Sheria za usalama barabarani wanasababisha uharibifu wa Mali za umma ikiwemo magari kujaribika ulemavu kwa viongozi Jambo ambalo halikubaliki.

Awali mwenyekiti wa chama Cha Madereva wa serikali Nchini, Charles Peter alikiri kuwepo kwa baadhi ya madereva wenzake wa serikali wasiozingatia sheria za usalama barabarani na kusema kuwa njia sahihi ya kuepuka ajali ni Madereva hao kushiriki mafunzo yanayotolewana chama hicho ili kuwasaidia kuwajengea uwezo.

"Madereva wote wa serikali nchi nzima katika mwezi huu wa pili ambao ni mwezi wa wiki ya nenda kwa usalama tujitathimini kwa kufuata sheria tusifuate kauli za mabosi wetu  ,bosi akikulazimisha kukimbia ,zingatia sheria"alisema

Aliongeza kuwa chama chao kimekuwa kikiwachukulia hatua baadhi ya Madereva wake wanaoenda kinyume cha sheria ila hatua ya mwisho inabaki kwa mwajiri wake ambaye ndio mwenye mamlaka zaidi ya kumfukuza au kuendelea naye.

Naye mwenyekiti wa madereva wa serikali Mkoa wa Arusha,Festo Kiteve alisema ajali nyingine  zinatokana na baadhi ya Madereva kutokuwa na uzoefu na magari  mapya ya kisasa yanayoletwa na serikali na kutoa rai kwa Madereva hao kushiriki mafunzo kabla ya kukabidhiwa gari .

"Madereva wapya wanaoajiriwa wahakikishe wanashiriki mafunzo muhimu ya udereva kwa ajili ya kumudu kuendesha magari ya kisasa kabla ya kuanza kazi "alisema.

Mmoja ya Madereva hao ,Hemedi Msemo  kutoka halmashauri ya wilaya ya karatu ,aliwashauri Madereva wenzake kushiriki mafunzo ya udereva na kuepuka kulazimishwa na viongozi kuendesha mwendo usiofaa.

Msemo ambaye anazaidi ya miaka 30 akiendesha magari serikalini, alisema hajawahi kupata ajali na Siri ya mafanikio katika kazi yake ni kuzingatia sheria za usalama barabarani pamoja na kutoogopa kutoa ushauri mzuri kwa kiongozi anayemwendesha.


Comments