SUMA JKT WADAIWA KUHUSIKA NA KIFO CHA RAIA ARUSHA.

 Mauaji tena Arusha,askari wa Suma Jkt wadaiwa kusababisha kifo cha raia.

Mwandishi wetu,Arusha

 Baadhi ya walinzi wa shamba la maua la kampuni ya Kiliflora  ambao ni askari wa  shirika la uzalishaji Mali   la jeshi la kujenga Taifa(SUMA  JKT) ,wanadaiwa kusababisha kifo cha mkazi wa Chekereni wilayani Arumeru mkoani Arusha. 

Askari hao wanadaiwa kusababisha kifo cha Richard Saibulu   wakimtuhumu kuvamia ndani ya shamba hilo na kutaka kuiba mbao za mirunda.

 Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha (RPC),Justine Maseju ametafutwa kuthibitisha tukio hilo lakini hajapatikana ofisini kwake na simu yake ya mkononi imeita bila kupokelewa.

Hatahivyo,mkaguzi mkuu wa Suma JKT kanda ya kazkazini,Emmanuel Awe amekanusha taarifa hizo huku akisisitiza askari wake hawahusiki na tukio hilo kwa namna yoyote.

 Akihojiwa na waandishi wa habari kaka wa marehemu,Geophrey Saibulu alisema kwamba juzi majira ya saa 11 jioni alipokea simu kutoka kwa mmoja wa askari aliyekuwa zamu na kumueleza kwamba kwamba marehemu mdogo wake yuko mahututi ndani ya shamba hilo kufuatia kipigo kikali kutoka kwa askari.

Saibulu,alisema kwamba alifika eneo la tukio na kuwauliza askari waliokuwepo ambapo walimwambia kuwa marehemu amepelekwa kituo cha polisi cha Chekereni ambapo alifika lakini akaambiwa hajaonekana kituoni hapo.

alisema kuwa Mara baada ya taarifa hiyo yeye na wenzake waliungana kweda hospitali ya Tengeru na hospitali ya mkoa  Arusha ya Mt Meru bila mafanikio na ndipo wakaamua kwenda kituo cha polisi cha Usariver.

"Mara baada ya kuzunguka katika hospitali ya Tengeru na Mt Meru bila mafanikio ikatubidi twende kituo cha polisi cha Usariver ambapo hatumkuta marehemu" alisema Saibulu

Naye mjomba wa marehemu,Peter Kivuyo alieleza kwamba wakiwa katika harakati za kumtafuta majira ya saa kumi jioni walipokea simu kwamba kuna mwili umefikishwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na gari la polisi na kisha kuhifadhiwa .


"Tukiwa kwenye harakati za kumtafuta ndipo tulipokea simu kutoka kwa askari mmojawapo  wa Suma Jkt kwamba mwili umepelekwa chumba cha kuhifadhia maiti Mt Meru na gari la polisi " alisema Kivuyo

Hatahivyo,Kivuyo alisema kwamba walipofika kuutambua mwili huo walimtabua marehemu ndugu yao huku mwili wake ukiwa umeharibika kwa majeraha usoni na sehemu mbalimbali mwilini.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Olomitu,Richard Gama alisema kuna mgogoro mkubwa baina ya walinzi wa shamba hilo na wananchi ambapo pamoja na kufanya vikao mbalimbali vya usuluhishi lakini jitihada hizo zimegonga mwamba.

Elias Lesendu ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Chekereni  kumekuwa na hali ya sintofahamu kufutia mgogoro huo hali ambayo imepelekea chuki baina ya raia na askari wa Suma Jkt.


"Ukweli ni kwamba kuna biashara isiyo rasmi inayofanyika ndani ya mashamba ya maua ya mirunda baina ya askari na raia hii ndio inapelekea matatizo yote" alisema Lesendu 

Afisa mtendaji wa kijiji cha Mlangarini,Amina Kombo alipokea taarifa za tukio hilo kupitia kwa balozi wa mtaa huo na tayari ameshalifikisha suala hilo kwenye ngazi za juu.

Balozi wa mtaa wa Chekereni, Gilbert John alisema kwamba alifika eneo la tukio na kushuhudia askari wa Suma Jkt akiwa amepakiwa kwenye pikipiki akivuja damu ambapo baadhi ya askari waliokuwepo eneo la tukio walimweleza kuwa askari huyo alipigwa na raia usiku wa kuamkamia Jana.

"Nilivyofika pale langoni nilishuhudia askari akiwa amepakiwa kwenye pikipiki anavuja damu nikawauliza Richard yuko wapi wakanieleza hawajui" alieleza Balozi huyo 

Mama mzazi wa marehemu,Dina Midimi alishindwa kujizuia na kisha kuangua kilio huku akimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan aunde tume ya kuchunguza tukio hilo ili haki ipatikane.

Comments