OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YAOKOA TRILIONI 10

Na Lucas Myovela, ARUSHA 

KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria,Mary Makondo ameipongeza  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali  kwa kuisaidia serikali kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi na kufanikiwa kuokoa  mali na fedha zaidi ya Sh.Trilioni 10 tangu ofisi hiyo ianzishwe mwaka 2018.


Akizungumza  Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya mawakili  wa serikali,  yaliyoandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali,Makondo alisema mafunzo hayo ya siku nne,anaamini yatawajengea uwezo zaidi wa kuisimamia serikali katika utekelezaji  wa miradi mikubwa na ya kimkakati.

"Nawapongeza sana kusaidia serikali katika utekelezaji wa majukumu yake na kuokoa fedha hizi toka kwenye mashauri ya madai, ambazo zimesaidia  kuendelea kutumika katika ukuaji wa uchumi wetu,nyie ni watu muhimu sana kwenye ukuaji wa uchumi wetu na uboreshaji wa pato la Taifa,"alisema Makondo.


Makondo ameeleza kuwa uanzishwaji wa ofisi hiyo ulienda kuleta wabobezi,Tija na ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi yanayofunguliwa dhidi ya serikali,ambayo kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kusaidia kuokoa fedha hizi ambazo wasingesimama kwenye weledi wao wasingeokoa na zingepotea.

"Ofisi unapaswa kuahirikiana na Taasisi zote za serikali ambazo zipo kwenye mihimili hii mitatu yaani serikali yenyewe,Bunge na Mahakama,ili kuhakikisha maslahi ya wananchi na ndani ya nchi na nje yanalindwa ipasavyo,"alisema Makondo.


Aidha, aliwapongeza  kwa kuwa mstari wa mbele kutatua migogoro inayoibuka katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha maslahi ya nchi inalindwa.

Pia aliwataka kujiandaa ipasavyo katika kupata elimu na stadi ya utatuzi wa migogoro, kwa njia ya maridhiano,majadiliano na suluhisho inayoibuka kwenye Taasisi za ndani na nje ya nchi.


"Tumeshuhudia migogoro hii imekuwa ikiongezeka na nyie watu muhimu na serikali inatambua  mchango wenu mkubwa na wengine mnahusika kutoa ushahidi,uandaaji wa nyaraka na katika uendeshaji wa mashauri hayo,iwapo mtaandaa vizuri nyaraka pamoja nakutoa ushauri itasaidia serikali kuiepusha na ulipaji wa fidia kwa wadau,"alisema Makondo

Aidha Makondo aliongeza kuwa serikali itaendelea kuboresha na kuwajengea uwezo kupitia mafunzo hayo ambayo ni nyenzo muhimu katika uendeshaji wa mashauri na uandaaji wa nyaraka kwa niaba ya serikali na kuwataka kuendelea kuwa waadilifu na kufanyakazi kwa bidii na kuweka mbele uzalendo na utaifa.


"Ofisi ya Wakili mkuu wa serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kuokoa kiasi cha sh,Trilioni 10, ambazo serikali ilipaswa ilipe fidia kutokana na kesi mbalimbali zilizofunguliwa ndani na nje ya nchi  ikidaiwa fidia kutokana na migogoro mbalimbali inayoibuka katika mikataba mbalimbali"alisem Makondo.

Naye Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata alisema Ofisi yake imeshiriki kikamilifu katika kukuza uchumi ikiwemo kushiriki  kwenye utatuzi wa migogoro na mashauri  kwa wakati na kwa kushirikiana na vyombo vya utoaji haki,pamoja na kutoa ushauri kwa Mwanasheria Mkuu  na kutatua migogoro mbalimbali kwa njia ya majadiliano.


"Lakini tumeendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi kwa niaba ya serikali na Taasisi zake na kuokoa fedha na mali nyingine za serikali,ambazo watu wasiostahili wangeweza kulipwa,mfano tangu kuanzishwa ofisi hii,tumeokoa zaidi ya Sh.Trilioni 10 na fedha hizi zimeendelea kutumika katika utoaji wa huduma na kukuza uchumi wa nchi,"alisema Mlata

Malata aliongeza kuwa serikali ingeshindwa mashauri hayo,basi ingewajibika kuwalipa wadai fedha hizo na kushindwa kutoa huduma na kukuza uchumi kwa kutumia fedha hizo.


Aidha pamoja na mafanikio hayo wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi wenye stadi maalumu (Specialized Skills) katika maeneo mtambuka kama mafuta na gesi,usuluhishi wa kimataifa,majadiliano,upungufu wa watumishi,ikama ya ofisi inataka kuwa na watumishi 312 waliopo ni 174,hivyo wana upungufu wa watumishi  138.

Comments