PROF MKENDA AZUNDUA MRADI WA UJIFUNZAJI MASHULENI.

Posted by; Lucas Myovela

 ARUSHA

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amezindua  mradi wa kuimarisha ujifunzaji shule za msingi pamoja na shule za awali, Mradi uliofadhiliwa na benki ya Dunia kwa fedha za kitanzania shilingi Trilioni 1.15.


Akizindua mradi huo Mkoani Arusha Leo June 6, 2022 Profesa Mkenda alisema utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano  utaboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, ujuzi na ubora wa walimu katika ufundishaji, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa rasilimali za utoaji huduma ngazi A halmashauri.

“Katika maeneo haya matatu program hii tunaizindua leo itajikita katika afua mbalimbali mojawapo ikiwa ni kuboresha miundombinu ya shule za msingi kwa kuzingatia mahitaji hususan ujenzi wa madarasa, uimarishaji wa mpango wa shule salama, kuimarisha uwiano wa uandikiswaji wa wanafunzi wa elimu ya awali, kuboresha vifaa na njia za ufundishaji elimu ya awali, pamoja na kuimarisha na kuendelea mpango wa mafunzo ya walimu kazini,” Alisema Profesa Mkenda.

Pia Prof, Mkenda aliwasihi watendaji wote kutoka ngazi ya wizara pamoja na  taasisi watakaohusika na utekelezaji  wa mradi huo kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuhakikisha serikali inafikia vigezo na viwango vyote vilivyowekwa kila mwaka kwani kadiri watakavyokuwa wanatekeleza ndio fedha zitakavyokuwa zinaletwa ambapo wakitekeleza kwa kusuasua fedha zitaletwa kwa kusuasua.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI David Silinde alisema kuwa wizara yake ndio watekelezaji wakuu wa mradi huo ambapo wamepokea tangu wakati wa maandalizi hivyo watasimamia utekelezaji wake kwa kuzingatia vigezo vya utendaji ambapo wamejipanga kuwajengea uwezo wasimamizi wa mradio huo.

Kaimu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge inayojihusisha na masuala ya huduma na maendeleo ya jamii Aloyce Kamamba ameishukuri serikali kwa kuanzisha mradi huo lakini kutokana na walimu kufanya kazi kubwa ni vema ikaajiri walimu watakaokuja kuwahudumia watoto kwani miundombinu na walimu inaenda sambamba.

Kamishna wa Elimu kutoka wizara ya Elimu sayansi na teknolojia Dkt Lyabwene Mtahabwa alisema kuwa elimu ya awali na msingi ndio msingi hasa wa makuzi ya mtoto ambapo tabia zote nzuri na muhimu mtoto anazipata na kupitia mradi huo wataweza kupata na mradi huo ulitokana na changamoto zilizobainika katika uchambuzi wa taarifa za sekta ya elimu 2021ambazo sinaathiri utoaji wa elimu bora katika ngazi za elimu msingi.


Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Msingi ya Arusha ( Arusha School ) Bw Loriv Njoroloi, ameeleza kuwa kwa kuzinduliwa kwa mradi huo utasaidi mabiresho makubwa katika utoaji wa elimu hapa nchini na yeye kama mkuu wa shule ameshajipanga vyema na walimu wenzie kuhakikisha wanafanikisha wa mradi huo unatoa matokeo chanya kwa wanafunzi na serikali kama ilivyo kusudiwa.

"Sisi kama Arusha School tumejipanga vyema kuhakikisha wanafunzi wetu wananufaika kikamilifu ili kuondoa changqmoto za usomaji maana mtoto akijengwa mapema ndivyo anakuwa akifanya vizuri zaidi katika masomo yake na nina amini kwa pamoja tukishirikiana na wazazi katika hili basi taifa letu litapata wasomi wengi ambao ni chachu ya maendeleo katika nyanja mbali mbali". Alisema Njoroloi.

Comments