ASWEKWA JELA KIFUNGO CHA MAISHA.

AKUTWA NA HATIA YA ULAWITI NA UBAKAJI KWA MWANAFUNZI WA DARASA LA 3.


Na Lucas Myovela _ ARUSHA

Mahakama ya wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, imemuhukumu kifungo cha maisha jela,Fadhili Kivuyo (29) mkazi wa Olturumet wilayani humo baada ya kutenda makosa mawili ya kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa kike darasa la tatu mwenye umri wa miaka tisa.


Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Gwantwa Mwankunga, alisema kuwa mahakama hiyo ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kutenda makosa yote mawili kwa ushahidi usio acha shaka uliotolewa na upande wa jamhuri.

Fadhili Kivuyo, Mtuhumiwa aliyekutwa na makosa na kuhukumiwa kifungo cha maisha Jela.


Kesi hiyo namba 31/2021 mshtakiwa alitenda makosa mawili ambapo kosa la kwanza la ubakaji mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia.


Alisema kosa la pili ni kulawiti ambapo mahakama hiyo ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha maisha jela,ambapo katika adhabu hizo mshtakiwa atatumikia adhabu moja ya kifungo cha maisha jela 


Awali mwendesha mashtaka wa kesi hiyo,Lilian Mmasi aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia Kama hiyo, ukizingatia kwamba umri wa mtoto huyo ni mdogo na ameharibiwa kisaikolojia.


Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mwankuga alisema kuwa mnamo,Mei 19,2021 majira ya saa 2 usiku mshtakiwa, Fadhili Kivuyo maarufu kwa jina la Toll,akiwa mlinzi wa nyumba binafsi eneo hilo,alimrubuni mwanafunzi huyo ( jina limehifadhiwa) akiwa ametumwa dukani na mama yake na kumvutia katika eneo alilokuwa akilinda na kumfanyia vitendo vya ukatili kwa kumbaka na kumlawiti.


Baada ya hukumu hiyo mmoja ya watetezi wa haki za watoto Mkoani Arusha, Mama Hindu Mwego ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Center for women and children development (CWCD)aliishukuru mahakama hiyo kwa kutenda haki ,akidai hukumu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wote wenye tabia Kama hiyo.

Mtetezi wa haki za watoto Mama Hindu Mwego, Mkurugenzi wa shirika la (CWCD)

Aidha mama Hindu aliwatahadhalisha wenye tabia kama hiyo wakidhani mahakama zipo likizo kuwa ,watashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria na kuitaka jamii kuhakikisha inaungana kukemea matukio ya aina hiyo ambayo huachwa yamalizike kinyumbani au wahusika kushindwa kutoa ushahidi mahakamani.


"Sote tunatakiwa kuwa wamoja kupinga matukio kama haya, Rais wetu ameonyesha nia ya kupambana na majanga haya na hawa waarifu wajue hawa watoto hawana hatia hata kidogo, na niwaombe mahakama kwenye kesi kama hizi wasipindishe wawanyooshee sheria ili wao nao wakaweze kujitia huko magerezani". Alisema Hindu.


Naye afisa ustawi wa jamii katika halmashauri ya Arusha, Josina Mlaki pamoja na kuishukuru mahakama hiyo kwa kutenda haki alisema kuwa bado changamoto ya ukatili kwa watoto ni kubwa na kuwataka wazazi kuwa waangalifu na watoto wao maana matukio hayo yamezidi kuongezeka kwa mwaka 2020/2021.


"Kwanza naishukuru mahakama kwa kutenda haki na isifumbe macho juu ya matukio ya ukatili kama haya, Pili wazazi ndiyo walinzi wa watoto wao wajenge urafiki nao waondoe nadharia ya kuwatuma sehemu za mabali watoto wakiwa wenyewe hii bita ni yetu sote tupambane kwa pamoja ili kuimaliza". Alisema Mlaki.


Alisema katika halmashauri hiyo matukio ya ukatili ni mengi, hivyo aliiasa jamii kukomesha matukio hayo kwa kuwa mstari wa mbele kuwafichua wahakifu na kutoa ushahidi mahakamani.

Naye mama wa mtoto aliyefanyiwa ukatili,Ester Efrahim alisema kuwa siku ya tukio alimtuma mtoto wake dukani lakini alikaa kwa muda Bila kumwona na kuamua kutoa taarifa kwa balozi ambapo majira ya saa tatu usiku walifanikiwa kumkuta mtoto barabarani akilia kwa uchungu na kutetemeka .


Alisema kuwa baada ya kumhoji ,mtoto wake alieleza kuwa alichukuliwa na kuingizwa katika chumba cha mlinzi huyo kwa zaidi ya saa moja akimbaka na kumlawiti ndipo walipoamua kumpeleka kutibiwa hospitalini na kugundulika kuwa ameharibika vibaya sehemu zake za siri ambapo hadi hivi Sasa anatumia Pempazi kujistili kutokana na haja kubwa kutoka lenyewe muda wote.


Comments