PANGA LA AWESO LA MOTO

WATUMISHI WASIO WAJIBIKA KWA WANANCHI KUFYEKWA MCHANA MWEUPE.

Na Lucas Myovela_ Arusha.

Waziri wa Maji Mhe, Jumaa Aweso amesema kuwa wizara yake imeanza kufanya tathimini ya wafanyakazi wake kwa makundi ya uwajibikaji ili kubaini na kuweza kuwaondoa watumishi wa mamlaka hiyo wasiowajibika kutatua changamoto za maji kwa wananchi hapa nchini kwa maana wanataka kukwamisha juhudi za Mhe Rais Samia Suluhu Hassan za kuondoa changamoto ya maji kitaifa pamoja na kumtua mama ndoo kichwani.

Aidha ameagiza wakuu wa mabonde ya Maji hapa chini wasiotaka kutembelea maeneo yao ya kazi ili kuzuia uharibifu wa vyanzo vya Maji unaosababishwa na wananchi kuvamia vyanzo vya maji waondolewe.

Waziri Aweso ametoa kauli hiyo mapema Leo Agosti 26,2022, Wakati akizindua mradi wa uondoaji wa mchanga kwenye mto Nduruma unaotekelezwa na bonde la mto pangani na baadaye kuongea na wananchi wa kata za Mbughuni na Shangharai Burka,wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.


Alisema kuwa wananchi wamekuwa wakihusika katika uharibifu wa vyanzo vya Maji lakini wakuu wa mabonde wamebaki kimya wakisubiri kufyeka mazao ya wananchi ambayo yameoteshwa kwenye vyanzo vya Maji jambo ambalo alisema ni kinyume na utaratibu.

"Wakuu wa mabonde ambao ndiyo wakurugenzi wa mabo de ya mani hapa nchini wamekuwa wakikaa ofisini kucheza na Laptop hawatembelei maeneo yao ya kazi wakisubiri kufyeka mazao yaliyooteshwa baada ya wananchi kuvamia vyanzo vya Maji muda wote walikuwa wapi" alisema Aweso.


"Niwaombe wakuu wa Wilaya muwe makini na msicheke na watumishi wa maji lege lege kama wapo mniambie ili kama ni kuzinguana tuzinguane mchana kweupe maana wanachi wanataka maendeleo, Ukicheza na nyenyere anae kutambalia mapajani atakung'ata pabaya".Aliongeza Aweso

"Mhe Rais alitupatia maelekezo ya kumtua mwanamke ndoo kichwani na katika kuliondoa tatizo hilo lazima tukamilishe zoezi hili, Nataka niwahakikishie wana wa Arumeru na tanzania kwa ujumla sitakuwa kikwazo katika kuwaletea maendeleo ya maji maana ndiyo kazi yangu ambayo Rais ameniamini na kunipa nimsaidie na ninaifanya kwa wananchi asilimia miamoja kwa uaminifu". Alisisita Aweso.


Alisema wakuu wa mabonde lazima wajue mipaka ya maeneo yao ya kazi na washirikiane na mamlaka zingine na kuwashirikisha wananchi kuwaelimisha kuliko kusubiri kufyeka mazao yao.

Aidha Aweso aliongeza kuwa serikali imetoa kiasi cha shilingi Milioni 100 ili kuweza kutekeleza mradi huo na aliahidi kuongeza kiasi kingine kama hicho ili kukamilisha mradi huo,pia ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa kata hizo mbili kwa ajili ya kujengea vivuko na kujenga mahusiano.

Awali mkurugenzi wa bonde la pangani,Mhandisi Segule Segule ,anayetekeleza mradi huo ,aliishukuru serikali kwa kutoa kiasi cha sh,milioni 100 ,ili kufanikisha mradi huo ambapo kwa kipindi kirefu Mto huo umekuwa ukisababisha maafa kwa wananchi kuzingirwa na Maji na wakati mwingine husababisha hadi vifo kwa wananchi na kupelekea wanafunzi kutokwenda mashuleni.

Alisema kuwa watu zaidi ya 700 kila mwaka wamekuwa wakiathiriwa na Maji ya mto huo ambayo husambaa bila kufuata mkondo wake kutokana na kujaa mchanga wakati wa kipindi cha mvua za masika ,huku wakati wa kiangazi wananchi hao hukumbana na vumbi zito linalotokana na Maji hayo.


Diwani wa Kata ya Shangharai Burka John Eliau alisema kuwa wanawake zaidi ya 10 wa Kata hiyo wamepoteza maisha katika kipindi cha miaka mitano kutokana na maji ya mtò huo kuvamia makazi yao na wengine kusombwa na maji wakati wakivuka mto huo kwenda kujifungua.





Comments