WADAU WACHACHAMAA ULINZI WA TAARIFA ZAO MTANDAONI.

 WADAU WACHACHAMAA ULINZI WA TAARIFA/FARAGHA ZAO

Na Mwandishi wetu, Arusha


Wadau wa masuala ya mtandao wameanzisha kampeni ya ulinzi wa taarifa na faragha za watanzania (Data Protection & Privacy campaign in Tanzania) kwa lengo la kuelimisha na kuwakumbusha wabunge kutunga sheria.


Kampeni iliyoanza Julai mwaka huu, imeendeshwa kwenye vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook kupitia kurasa za ‘@ProtectDataTZ’.


Mratibu wa kampeni hiyo James Laurent alisema lengo la kuuelimisha umma wa watanzania ni ili kujikinga na changamoto sugu ya utumiwaji mbaya na kuvujishwa kwa taarifa nyeti za watu kinyume na idhini zao sambamba na kuliomba bunge na serikali kutunga sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu (Data Protection & Privacy law).  


James alisema kwenye mkutano wa jukwaa la usimamizi wa Intaneti Tanzania (Tanzania Internet Governance Forum) mwaka jana, Dkt. Jim Yonazi - katibu mkuu wa wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, alinukuliwa akisema utungwaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa, upo kwenye hatua za mwisho "hivyo kampeni hii imekuja muda mwafaka ambapo tunashuhudia wimbi kubwa la kuvujishwa kwa taarifa nyeti za watanzania pamoja na matumizi mabaya ya taarifa za umma pasina idhini za walengwa".


Alitaja baadhi ya mifano ya utumiwaji mbaya wa taarifa za watu ni pamoja na namba za simu za wateja wa mitandao ya simu, vitambulisho vya taifa (NIDA), vitambulisho vya mpiga kura, kadi za ATM, video na picha za udhalilishaji wa kingono almaarufu ‘Connection’, mazungumzo na meseji za siri, vyeti vya matokeo ya elimu, bila kusahau kero ya jumbe za “Ile pesa tuma kwenye namba hii", “Jiunge FREEMASON umiliki majumba, magali, pesa viwanja, ajira, ukue kibiashala, “Habari za leo mzazi mimi ni mwalimu naomba unipigie haraka sana shuleni kuna tatizo mtoto wako amedondoka ghafla kaumia sana”, “Mjukuu wangu ndagu niliyokukabizi hiyo uwe makini na pesa hizo zinazokuja usiogope ndio mafanikio yako, si nilikwambia utafanikiwa kwa mda mfupi sasa umeona mwenyewe na siri hiyo usitowe kwa mtu yoyote utajili huo ni mkubwa sana utaweza kuweka miladi ya kira aina popote pale unipigie nikuelekeze.” 


"Hizo ni baadhi tu ya jumbe za kitapeli ambazo wateja wa mitandao ya simu hupokea kila siku, kupitia kampeni ya ulinzi wa taarifa na faragha za watanzania, tunauelimisha umma kuhusu udanganyifu wa hawa matapeli licha ya SMS hizi kuwa na makosa mengi ya kiuandishi lakini tamaa za watu kutaka kutajirika haraka, ama upendo wa wazazi kwa watoto wao huwafanya wakurupuke kutuma pesa" alifafanua na kuongeza kuwa,


"Utaratibu wa kusajili namba za simu kwa alama za vidole na namba za vitambulisho vya taifa (NIDA) ulipoanzishwa nchini mwaka 2018, binafsi nilidhani ungekuwa mwarobaini wa utapeli kwa njia ya namba za simu. Hata hivyo, matapeli wameongezeka maradufu licha ya jitihada nyingi za jeshi la polisi Tanzania kukamata mitandao ya matapeli hawa pamoja na kuwaonya watumiaji wa mitandao ya simu mara kwa mara dhidi ya utapeli wa namna hii kupitia huduma ya kuripoti UTAPELI kwa namba 15040 au kwa kupiga *148*90#".


Kupitia mijadala ya kila wiki inayofanyika kwenye Twitter Space ya ukurasa wa @ProtectDataTZ, mmoja wa wachangiaji wa mada kuhusu meseji za utapeli Ashraf Ramadhan alihoji, “Kwanini mitandao ya simu kwa kushirikiana na mamlaka ya mawasiliano (TCRA) wasizuie hizo SMS juu kwa juu kabla hazijamfikia mteja?” na “hawa matapeli wanapata wapi namba zetu za simu?” na "kama namba zote za simu huwa zinasajiliwa kwa vitambulisho vya taifa (NIDA) na alama za vidole, kwanini mitandao ya simu haifungii namba za matapeli?". 


Janeth Joseph alihoji “hawa watu [matapeli] najiuliza huwa wanapata wapi namba zetu?…Huenda ni watu waliowahi kufanya kazi kwenye kampuni za mitandao ya simu na baadae wanaanza kuvujisha siri za kampuni, kwahio wanatumia data za wateja na kufanya utapeli hivyo sheria ni muhimu sana kwenye hili. 


Majirani zetu Kenya na Uganda tayari wana sheria hii, ulinzi dhidi ya udhalilishwaji wa kingono, sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za watu pia itawalinda wahanga wa udhalilishaji wa kingono mitandaoni almaarufu ‘Connection’, wengi wao wakiwa wanawake lakini pia kuwapa adhabu kali wanaovujisha maudhui ya udhalilishaji wa kingono mitandaoni na nje ya mitandao.


Hata hivyo kampeni hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa karibu na wadau wa haki za kidijitali na haki za kijinsia; Peter Mmbando - Digital Agenda for Tanzania Initiative (DA4TI), Imani Henrick - Mwandishi wa Habari, Idd Ninga - Dunia Salama Foundation (DUSAFO), Elizabeth James - Mwanasheria, Mihwela Justine - ATPWE na wadau wengine .

Comments