MKURUGENZI MAULY TOUR ALAMBA UBALOZI MDOGO

MKURUGENZI KAMPUNI ILIYOSHIRIKI KUTENGENEZA ROYAL TOUR APEWA UBALOZI

Lucas Myovela.

Kulia ni balozi wa Brazil nchini Tanzania Balozi Antonio Augusto Martins Cesar akimkabidhi cheti cha ubalozi mdogo Mozzah Mauly kusimamia mikoa ya Kaskakazini na kanda ya ziwa nchini Tanzania.


Ubalozi wa Brazil nchini Tanzania umemteua Mkurugenzi wa kampuni ya Mauly tours and Safari Mozzah Mauly kuwa balozi mdogo wa jamhuri ya nchi hiyo kuhudumu mikoa ya kaskakazini na kanda ya ziwa nchini Tanzania.


Akizungumza wakati wa hafla ya kupewa cheti cha utambulisho na balozi wa Brazil nchini Tanzania Balozi Antonio Augusto Martins Cesar amesema anashukuru kwa Mozzah kukubali changamoto hii mpya kwake ya kusimamia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Simiyu na Mwanza.


"Mwaka huu tumeanza vizuri kwa kuwa na mahusiano na Mauly tours hasa Mozzah na naishi Tanzania kwa kujiamini kwa sababu nina watu nyuma yangu na kwa kipindi cha miaka 10 niliyoishi Tanzania najivunia kuongeza wigo wa ushirikiano" Amesema balozi Antonio.


Amesema kuwa aliutambua umahiri na utendaji kazi wa familia ya Mauly alipokuwa na kazi maalumu (project) kwenye hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ngorongoro hivyo hana wasiwasi na usimamizi wa mikoa hiyo.


Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya Mauly tours, Mozzah Mauly ameshukuru wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki kwa uteuzi na kuona anauwezo wa kuhudumu eneo hilo.


"Nimejiona wa pekee kwa uteuzi uliofanyika, na naahidi kutoa ushirikiano mzuri wa mataifa haya mawili yaliyoniamini" amesema Mozzah, na kuongeza.


"Jambo hili ili lifanikiwe halitakuwa lakwangu peke yangu bali sote katika kupiga kila hatua ya mafanikio".


Mbali na hilo hakusita kumshukuru Mama yake, Dada zake na balozi Antonio kwa kile alichoeleza kuwa ni kumwamini na kumpa ushirikiano uliomfanya asimame na kukuza ushirikiano kati ya watu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na Brazil.


Kampuni ya Mauly tours and Safari ni miongoni mwa kampuni zilizoshiriki kutengeneza filamu ya kuhamasisha utalii na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasan (Tanzania The Royal Tour).

Comments