WALIYO FAULU MASOMO YA SAYANSI KUSOMESHWA BURE NA SERIKALI.

RAIS MWINYI ASEMA SERIKALI YAKE ITAENDELEA KUIPA KIPAUMBELE SEKTA YA ELIMU.


PROF MKENDA AWEKA WAZI WALIYO FAULU KIDATO CHA VI MASOMO YA SAYANSI KUSOMESHWA BURE NA SERIKALI KUPITIA MPANGO MAALUM WA "SAMIA SCHOLASHIP".

Na Lucas Myovela - Zanzibar.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt Hussein Ally Mwinyi amesema Serikali yake itaendelea kuipa kipaumbele cha kwanza Sekta ya Elimu kwa kueleza kuwa maendeleo yoyote hayawezi kupatikana pasipo watanzania kuwa na Elimu.

Rais Hussein Mwinyi amesema hayo mjini Zanzibar katika hafla ya ugawaji vishkwambi kwa walimu pamoja na kompyuta mpakato kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita kutoka skuli za Zanzibar ili kuwapa motisha wanafunzi ili kuweza kuendelea kufanya vizuri, Vishkwambi hivyo vimetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


Dkt, Mwinyi ameongeza kuwa anaamini vishkwambi hivyo vitasaidia kupiga hatua kwenye suala zima la TEHAMA katika sekta ya Elimu mjini Zanzibar na kuwataka walimu kuvitumia ipasavyo katika upanuzi wa wigo wa utoaji elimu.

"Ili nchi iwe na wataalamu ni lazima iwekeze kwa kiasi kikubwa kwenye elimu hivyo tutajipanga kutoa mafunzo kwa walimu waliopo na kuongeza wengine ili tuzalishe wataalamu watakaoiinua nchi," amesema Rais Mwinyi.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara ya Elimu Bara na Zanzibar zinafanya kazi kwa kushirikiana katika suala la mageuzi ya Sera ya Elimu na maboresho ya mitaala ili kuwawezesha vijana wa pande zote mbili kupata ujuzi na stadi zitakazowasaidia kujiari ama kuajiriwa na kuchangia katika uchumi wa Taifa.

Prof, Mkenda amesema anaamini mapendekezo yatakayotolewa na Serikali baada ya kupokea maoni ya wadau yatashabihiana isipokuwa tu pale ambapo mazingira yatahitaji kuwe na tofauti.


"Kuhusu suala la mageuzi ya elimu naamini hakutakuwa na tofauti kubwa kati ya Elimu ya Bara na ya Visiwani kwa kuwa kazi ya mapitio ya Sera na mitaala imefanywa kwa ushirikiano wa pande zote mbili" amesema Prof. Mkenda.

Kuhusu ugawaji wa Vishikwambi, Prof. Mkenda amesema Serikali imetoa vishkwambi 6,600 kwa walimu upande wa zanzibar ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa kugawa vishkwambi kwa walimu wote nchini katika kutambua umuhimu wa TEHAMA kwenye ufundishaji na ujifunzaji. 


Aidha Prof, Mkenda ameongeza kuwa kitendo cha Rais Mwinyi kutoa motisha ya kompyuta kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitachochea juhudi za wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na hivyo kuwa tayari kujenga Taifa.

"Niwapongeze sana baadhi ya wanafunzi mliyo wezakupata kompyuta hizi hasa wanafunzi wa kidato cha sita ambao mmefaulu vizuri masomo ya sayansi mmekuwa wanufaika wakubwa hasa katika ofa ya elimu maalufu kama "Samia Scholarship" hivyo watasomeshwa bure na Serikali kupitia mpango huo maalu.

Kwa upande wake Mhe. Lela Mohamed Mussa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ameshukuru kwa kupokea vishkwambi hivyo 6,600 na kwamba vitagawiwa kwa Walimu wa shule za Msingi na Sekondari za umma ili wavitumie kama zana za kufundishia na kujifunzia.

Comments