JIJI LA ARUSHA LA MWAGA MABILIONI KWA WANAWAKE, VIJANA NA WALEMAVU.

SASA KILA KITU NI KIDIGITALI, WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA MIPANGO MADHUBUTI, MAPATO YAPANDA KUTOA BILIONI 30 HADI 60.

Na Lucas Myovela_Arusha

Jiji la Arusha limetoa mikopo ya asilimia kumi ya Shilingi Bilioni 2.656 Kwa vikundi 169 kwaajili ya makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu katika Jiji la Arusha.


Aidha Watu wenye ulemavu wanaruhusiwa kukopa mikopo hiyo bila kuwa na kikundi na dirisha lipo wazi na kusisitiza Jiji litaendelea kutoa mikopo kwa njia ya mtandao ili kupata takwimu sahihi za wanufaika wa mikopo hiyo.

Akiongoza zoezi hilo la utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu,Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa amesisitiza wanaopewa mikopo hiyo kuwa wafanyabiashara wenye ubunifu na kuacha biashara za mazoea zinazo pelekea kukata kwa mitaji yao.


Dc Mtahengerwa amesisitiza kuwa endapo wanufaika wa mikopo hiyo wakiwa wabunifu wataongeza tija katika biashara zao ikiwemo kufungua fursa za kutangaza biashara zao ili kupata soko la ndani na hata nje ya mkoa wa Arusha.

"Endapo mikopo hii iliyotolewa na Jiji letu itafanyiwa kazi kwa kina itawapelekea kujikwamua kiuchumi na kutoa mwangaza kwa wapewa mikopo kutojionyesha kuwa wanahela bali wafanye kazi kwa bidii ili kuleta tija na kujikwamua kiuchumi kama yalivyo malengo na matalajio ya Taifa". Amesema Dc Mtahengerwa.

"Pia niwaombe Kinababa wake zenu wakipata mikopo msiwazuie kufanya biashara zao wala kuwaibia, waacheni wabuni biashara zao ili wajikwamue kiuchumi kwani wanawake wa Arusha na makundi maalum ni wachakarikaji katika kujikwamua kiuchumi na wanaweza wanapowezeshwa kama hivi ambavyo jiji limewawezesha vyema". Aliongeza Mtahengerwa

Aidha Mtahengerwa ameeleza kuwa uombaji mikopo kwa njia ya kieletroniki (mtandao ) ni mzuri kwani unaonyesha vikundi vingapi vimepata mikopo na vipo wapi hivyo Jiji litaendelea kutoa mikopo kwanjia hiyo ili kujua makundi yaliyofikiwa katika utoaji na ujeshwaji wa mikopo na ameweza kumshukuru Rais wa Jamuhiri ya muungano wa Tanzania Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwakwamua wananchi katika hali ya chini na kufungua fursa za kibiashara.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Hargeney Chitukuro amesema mikopo hiyo haijapata kutokea na nimatumaini yake kuwa mikopo hiyo itaenda kwa vikundi saba, viwanda vidogo 28, wasafirishaji 77, wakulima na wafugaji na vikundi 169 vya kada mbalimbali ikiwemo wanawake,walemavu pamoja na vijana.

"Tangu mwaka jana hadi sasa Jiji la Arusha limetoa mikopo ya Shilingi Bilioni 3,934,133,800 hadi sasa vikundi vilivyofikiwa kwa utoaji wa mikopo kwenye vikundi 339 na vikundi hivyo vimeweza kuzalisha ajira zaidi ya 1,965 kwa watanzania". Amesema Mkurugenzi Chitukuro.

Akitoa mchanganuo wa mkopo huo Meya wa Jiji hilo Ndg, Maximilian Irrange amesema shilingi Bilioni 1.953 zimeenda kwenye vikundi 127 vya wakina mama ( wanawake), na shilingi milioni 602 zimeenda kwa vikundi 32 vya vijana pamoja na Shilingi Milioni 100 zimeenda kwa vikundi 10 vya walemavu.


 Pia Maximilian ameweza kuwahasa vijana wanaochukua mikopo hiyo iwe yenye tija na kupelekea watu wengine wakope ikiwemo urejeshwaji mzuri wa marejesho na siyo kwenda kuzifanyia anasa.

"Msioe kwa hela za mikopo Jiji limejitahidi na Kaimu Mkurugenzi Chitukuro unajitahidi sana sana katika kuhakikisha mikopo inatoka kwa wakati lakini nyie mnaopewa mikopo hakikisheni mnarejesha kwa wakati". Amesema Irrange.


"Rai yangu kwa wale waliyokopa wafanye marejesho kwa wakati maana kabla hatujawapa pesa hizi walipata semina mahususi namna ya kutumia mikopo hii, Lengo letu ni kutengeneza na kupanua wigo wa watu wa daraja la kati kiuchumi na wale waliyo pata wafanye marejesho kwa wakati ili ziweze kusaidia wengine". Ameongeza Irrange

Aidha Irrange amesema kwamba mapato ya Jiji la Arusha yameongezeka kwa 100% kutoka Bilioni 30.5 kwa mwaka fedha 2022 /2023 kwenda Bilioni 60.6 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, na hayo yote yanatokana na sera nzuri ya Mhe, Rais Samia Suluhu Hassan na pia kwa kupanda kwa mapato hayo itapelekea Jiji hilo kukua zaidi katika uboreshaji wa mambo mbali mbali ya kimaendeleo.


"Wananchi wa Jiji la Arusha wategemee kuiona Arusha Mpya yenye maendeleo makubwa na mipango sahihi ya jiji letu na kuwaka taa mitaa yote ya mjini maana tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwaajili ya kuweka taa za barabarani na muda wowote kuanzia sasa tenda hiyo itatangazwa". Amesema Irrange.








Comments