JANGILI SUGU WA MUDA MREFU WA KUUWA TWIGA AKAMATWA BURUNGE WMA.

 Mtuhumiwa wa ujangili wa Twiga akamatwa Burunge WMA

Na Mwandishi wetu , Babati

Mtuhumiwa wa ujangili wa Twiga ambaye amekuwa akisakwa kwa muda mrefu na askari wa Wanyamapori katika hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge, wilayani Babati mkoa Manyara Amos Benard Meja amekamatwa Jana usiku.


Mtuhumiwa huyo amekamatwa kutokana na mtego ulioandaliwa na askari wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA),Askari wa Burunge WMA na askari wa Taasisi ya Chem chem association ambayo imewekeza shughuli za Utalii katika eneo hilo.


 Meja ambaye amekuwa akisakwa kwa tuhuma za uwindaji wa Twiga na kuuza Nyama maeneo mbalimbali amekamatwa majira ya saa kumi na moja jioni maeneo ya mfulwang'ombe kwenye Kambi ya samaki.


Mtuhumiwa huyo ambaye haikuwa rahisi kutiwa nguvuni alikamatwa na kikosi cha askari maalum wa Wanyamapori James Misuka,Samweli Bayo,Khamis Chamkulu,Mohamed Abdallah,Pascal Mandao,Emmanuel Duxo,Wilfred Ngitoor na Karoli Umbe baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasiri.


Mwendesha Mashitaka wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) Getrude Kariongi alikiri Jana kukamatwa mtuhumiwa huyo.


"Ni kweli amekamatwa huyu mtuhumiwa alikuwa anakabiliwa na kesi kadhaa za ujangili na tayari amekabidhiwa polisi"amesema.


Meneja wa Chem chem association, Clever Zulu amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni jitihada ambazo zimefanywa na askari wa Wanyamapori.


Zulu amesema askari hao wa Wanyamapori walipata mafunzo maalum kutoka kwa maafisa wa TAWA jinsi ya kufanya upelelezi,upekuzi na ukamataji wa majangili.


"Haya ni mafanikio makubwa kwetu katika kulinda rasilimali tunawapongeza askari kwa kuonesha ufanisi baada ya mafunzo"amesema


Zulu amesema Chem chem association ambayo inatumia zaidi ya sh 400 milioni kila mwaka katika kupambana na ujangili katika eneo la Burunge WMA Itaendelea kutoa fedha za kupambana na ujangili.


Eneo la Burunge WMA kumekuwepo na matukio mengi ya ujangili wa Twiga kutokana na eneo hilo kuwa na idadi kubwa la Twiga kutokana na kuimarika uhifadhi.


Pichani ni mtuhumiwa wa ujangili wa twiga aliye kamatwa.

Comments