NACTVET KUENDELEA KUSIMAMIA VYUO VYA UFUNDI ILI KUPATA ELIMU YENYE TIJA YA KUJIBU CHANGAMOTO.
Na Lucas Myovela _ Arusha.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali ipo katika mchakato wa kupitia mabadliko ya mtaala wa elimu hapa nchi kuanzia Januari 2024, mambadiliko hayo ambayo yatakuwa wezeshi kwa wanafunzi kufanya maamuzi mapema.
Prof, Mkenda ameyasema hayo jana Mei 19,2023 Jijini Arusha wakati akifungua maonyesho ya Pili ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yanayoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Prof, Mkenda ameeleza kuwa kutokana na maonyesho hayo yamekuwa ni chachu kubwa kwa taifa na watayaunganisha ili yazidi kutoa manufaa makubwa kwa taifa na kufikia mafanikio makubwa ya kielimu pamoja na elimu ya ufundi stadi.
"Mabadiliko makubwa ya mtaala wa elimu yanakuja kuanzia Januari 2024, ambapo elimu ya msingi itakuwa kwa miaka 6 na elimu ya sekondari itakuwa ya miaka minne na kufanya jumla miaka ya kupata elimu kuwa 10 kulinganisha na sasa". Amesema Prof Mkenda.
"Ndani ya miaka 6 tutapunguza baadhi ya masomo na kuweka mkazo zaidi katika somo la kingereza kuanzia shule ya msingi hadi sekondari". Aliongeza Mkenda.
Aidha Prof, Mkenda alisema kwamba kwa upande wa elimu ya sekondari itakuwa na mikondo miwili ambapo kutakuwa na mkondo wa elimu ya jumla na mkondo wa elimu ya ufundi stadi, Pia vyuoni kutakuwa na elimu ya jumla na elimu ya ufundi stadi ili kuzidi kukuza ujuzi kwa wanafunzi.
" Katika elimu ya sekondari hapa kutakuwa na mikondo miwili ambayo itamfanya mwanafunzi achague mwenyewe anata kusomea nini, Mkondo wa kwamza utakuwa ni wa elimu Jumla hii itakuwa ni masomo ya kawaida na Mkondo wa pili utakuwa ni elimu ya ufundi stadi huu utakuwa unafundisha elimu ya ufundi moja kwa moja na itakuwa na michepuo ya taaluma ya ujuzi ya mwanafunzi aliyo chagua". Amesema Prof, Mkenda.
"Mchepua huu wa elimu ya ufundi unamuwezesha mwanafunzi kusome fani yoyote anayo ipenda lengo likiwa ni kukuza vipaji kwa wanafunzi wakiwa bado wadogo ili kuzidi kuwaongeza bunifu katika vipawa vyao na wakimaliza elimu hii ya ufundi pia wataendelea na vyuo ambapo pia watakuna na elimu chuoni inayo fundisha ufundi stadi na kuendeleza vipaji vyao". Alisema Prof Mkenda.
"Tumeona haya yanaweza kusaidia taifa na kuongeza chachu kwa vijana ambapo watakuwa na ujuzi mkubwa utakao wasaidia kujiajiri na kulionda taifa katika wimbi la ukosefu wa ajira". Aliongeza Prof, Mkenda
Aidha pia Prof, Mkenda aliwapongeza NACTVET kwa kuendela kufanya maonyesho hayo maana yanaunganisha Vyuo vya ufundi, juhudi za ubunifu, sayansi na teknolojia pamoja na shughuli za uzalishaji na huduma kwa ajili ya kutengeneza uwezo wa kutambua mahitaji na kuimarisha utoaji mafunzo kwa vitendo kwa vijana.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu la Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt, Adolf Rutayuga amesema kuwa nchi nyingi Duniani zinatambua kuwa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya viwanda, hivyo inapaswa kuzingatia umahiri wa kutenda na mahitaji ya soko la ajira kwa wahitimu.
Pia Dkt, Rutayuga ameongeza kuwa ili kuwepo na elimu yenye tija inayojibu changamoto za jamii ni lazima kuwepo na mashirikiano kati ya watoa mafunzo pamoja na waajiri ili kisaidia vijana kufanya kazi wanapo maliza mafunzo yao na kutoa mchango kwa taifa.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Husna Sekiboko ameishukuru Wizara ya elimu kwa kuishirikisha Kamati hiyo katika shughuli zote za Wizara na kuahidi kwamba itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mageuzi makubwa ya elimu yanayotarajiwa yanatokea.
Pia Mhe, Husna amese kuwa maonesho ya NACTVET ni mazuri na kuwaomba wananchi kujitokeza na kutembelea maonyesho hayo ili kuona namna kazi kubwa ya ubunifu na ufundi zinazofanyika katika Vyuo na Taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya ufundi hapa nchini.
Naye mmoja wa wadhamini Deogratius Haule kutoka Geita Gold Mine amesema wataendelea kudhamini maonesho hayo ili vijana wa Vyuo vya kati na Taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo zipate fursa ya kuonyesha uwezo, vipaji na ubunifu wanaofanya na hivyo kuleta maana halisi ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Maonesho ya Pili ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yanayoendelea jijini Arusha yameshirikisha zaidi ya Taasisi 200 zikiwa ni Vyuo vya elimu ya ufundi, ufundi stadi, Vyuo vikuu, Taasisi na Makampuni ya waajiri, wajasiliamali na vikundi mbalimbali vinavyofaidika na elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi hapa nchini
Comments
Post a Comment