WATUMISHI WA WIZARA YA MADINI ZINGATIENI UADILIFU, WELEDI NA UWAJIBIKAJI.

 MBIBO, AMEWATAKA WATUMISHI MADINI KUZINGATIA UADILIFU, WELEDI NA UWAJIBIKAJI.

Mpaka sasa Kagera imefikia lengo la asilimia 71.13 ya makusanyo ya maduhuli ya Serikali.

Na Mwandishi wetu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewataka watumishi wa Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Kagera kuwa waadilifu na wazalendo katika uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu yao.


Mbibo ametoa wito huo baada ya kutembelea Kituo cha Umahiri cha Kagera kilichojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.08 kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo kujifunza namna bora ya shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

"Hatuwezi kusimamia Wizara ya Madini kama hatuna weledi, uadilifu na uwajibikaji na tukizingatia kwamba sekta hii ndiyo sekta inayoongoza kwa kuuza bidhaa zitokanazo na madini nje ya nchi," amesema Mbibo.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kagera Samwel Shoo amesema, mkoa wake umepewa lengo la kukusanya maduhuli ya Serikali ya kiasi cha shilingi bilioni 7.48 ambapo mpaka Aprili 30, 2023 mkoa huo umekusanya kiasi cha shilingi bilioni 5.32 sawa na asilimia 71.13 ya lengo.


Shughuli za uchimbaji wa madini zinazidi kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa madini unaofanywa mkoani humo ni madini ya dhahabu, bati ghafi na madini ya ujenzi.


Pamoja na mafanikio hayo, Shoo amesema ofisi yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa vyombo vya usafiri ikiwemo magari na pikipiki, vitendea kazi kama kompyuta na samani za ofisini pamoja na upungufu wa rasilimali watu. 

Awali, Mbibo alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na kuzungumza na Katibu Tawala wa Mkoa huo Toba Nguvila ambapo alipata taarifa za madini za mkoa huo ikiwemo changamotbo za ukosefu wa nishati ya umeme katika migodi iliopo mkoani humo.


"Mkoa wa Kagera uko salama hususan katika sekta ya Madini na tuna mkakati wa kuhamasisha madini ya nchini za jirani ikiwemo Kongo kuuza madini yake katika soko letu la Kagera kwa lengo la kuongeza makusanyo ya mkoa na serikali kwa ujumla," amesema Nguvila.

Vituo vya Umahiri vitajengwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Kagera, Bariadi, Musoma, Chunya, Songea, Mpanda na Handeni.

Comments