KITALU B ILIKIUKA KANUNI ZA UCHIMBAJI WA MADINI.

ONYO KALI LA TOLEWA KWA WACHIMBAJI WENGINE WANAO ZENGEA KITALU C NA MIGODI MINGINE.

Na Lucas Myovela - Mirerani.

Kampuni ya Gem & Rocky Venture inayochimba madini ya Tanzanite kitalu B katika Mji wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara imetakiwa kuchimba madini hayo kwa kufuata leseni waliyopewa na sio vinginevyo.


Hayo yameelezwa na Afisa Mfawidhi wa Madini Kanda ya Mirerani, Mernad Msengi baada ya ukaguzi wa mipaka ya kampuni hiyo dhidi ya Kitalu C kinachomilikiwa na Mwekezaji Onesmo Mbise kwa ubia na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Msengi ameeleza kwamba uamuzi huo wa uhakiki wa mipaka yamekuja baada ya maamuzi ya rufaa ya kampuni ya Gem & Rock Venture iliyokatwa na Mkurugenzi wake Joel Mollel Saitoti maarufu kwa jina la Saitoti kutupiliwa mbali na wizara ya madini na kutakiwa kufuata sheria na kanuni za uchimbaji ikiwa ni pamoja na kurudi katika eneo sahihi la mgodi wake kama leseni yake inavyosema.

 

Msengi ameongeza kuwa mbali na swala la kuhakiki mipaka ya kila mgodi, Pia Saitoti ametakiwa kujenga ukuta ili kuweza kutenganisha mgodi wake na mgodi wa kitalu C na kuhakikisha anarudi nyuma umbali wa mita 650 alizo kuwa amezidi hadi eneo lake la uchimbaji wa kitalu B kwa mujibu wa leseni ya mgodi wa Rocky & Venture.


Aidha Afisa Madini huyo ametoa rai kwa wamiliki wote wa migodi ya Tanzanite Mirerani kuheshimu sheria na kanuni za madini pia kuchimba eneo ambalo leseni inaruhusu vinginevyo hatua kali zitachukuliwa ka wale wanaokiuka taratibu kwa makusudi.


"Nipende kuwaonya wachimbaji wote wa madini ya Tanzanite hapa Mirerani kufuata sheria na kanuni za uchimbaji kutokana na leseni zao walizo pewa za uchimbaji kwa kuzingatia mipaka, Serikali inayo nia thabiti ya kuendelea kushishirikiana na wachimbaji wote wa madini ili kukuza sekta ya madini na uchumi kwa ujumla kwa ustawi wa taifa letu". Amesema Msengi.


"Niwaombe tu wamiliki wote wachimbe kwenye maeneo yao ya mgodi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima naamini kila mgodi unazalisha kwa wakati wake na siyo kitu kizuri kutoa eneo la mgodi wa mwenzio ili kupata madini hili halitavumilika sheria zipo wazi hautwaachwa lazima sheria ichukue mkondo wake". Ameongeza Msengi.


Awali kamati maalumu mnanmo tarehe 28 march 2023, ilitoa taarifa kuwa Gem & Rock Venture ilifanya makosa katika uchimbaji kwa kuingia ndani ya kitalu C zaidi ya mita 650 na kufanikiwa kufanya uzalishaji wa zaidi ya kilo 4 za madini ya Tanzanite kinyume na taratibu na kufanya uhalibifu hatua ambayo kampuni hiyo ilipinga na kukata rufaa kwa katika Mkuu wa Wizara lakini hiyo ilitupiliwa mbali.


Comments