NEEMA KWA WALIMU KULIPWA MADENI YAO YOTE:

Ndani ya Siku 7 Madeni yote ya Walimu yawe yamewasilishwa Ofisi ya Rais Tamisemi.

Na Lucas Myovela

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayesimamia elimu, Dkt. Charles Msonde ameagiza Maafisa Elimu wa Wilaya nchini kubainisha madeni yote ya Waalimu na kuyawasilisha Ofisi ya Rais TAMISEMI. 


Dkt. Msonde ameeleza hayo leo tarehe 04 June 2023 wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Elimu wa Wilaya na Mikoa yote nchini cha kujadili na kutathmini utekelezaji wa vigezo vya upimaji wa elimu nchini (KPI) kilichofanyika Mkoani Tabora.

“Maafisa Elimu na Wakuu wa Idara wa Halmashauri tunawapa wiki moja mtuletee taarifa ya madeni yote ya Walimu ikiwa ni pamoja na ya likizo na Uhamisho kwa kuyapanga kwa mwaka, na kila fedha inayoletwa kwa mwezi katika Halmashauri ya kulipa hayo madeni nijulishwe Waalimu wangapi wamelipwa na madeni yamebakia kiasi gani” amesema Dkt. Msonde.


Msonde amesema Serikali imekuwa ikitenga na kutoa fedha za likizo na Uhamisho kila mara lakini fedha hiyo imekuwa haitolewi kwa haki ambapo yamekuwa yakilipwa madeni ya hivi karibu na madeni ya kipindi cha nyuma yanaachwa.

“Madeni haya tukiyalipa kwa haki, Waalimu watapata faraja na kujua kuwa Serikali yao inawajali na imelipa madeni kiasi flani kwa mwaka husika na mwaka unaofuata Serikali itaendelea kupunguza madeni hayo kwa Walimu wetu” amesema Msonde.


Aidha, Dkt. Msonde amesema Serikali inayoonzozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina uwezo na imedhamiris kumaliza na kuondoa kero zote ikiwa ni pamoja na madeni yote ya Walimu ili waweze kufanya kazi kwa weledi na utulivu.

Kadhalika, amekemea tabia ya baadhi ya Maafisa Elimu kuwanyanyasa viongozi walio chini yao pamoja na Waalimu na kueleza kuwa Serikali haitamfumbia macho yeyote atakayebainika.


“Viongozi wenzangu fanyeni kazi kwa ushirikiano na wasaidizi wenu, suala la mahusiano hafifu kati yenu na wasaidizi wenu na suala la kutowapa hadhi wasaidizi wenu kufanya kazi kwa molali, hilo ni kipimo chenu na linaweza kukutengua katika cheo chako”. Amesema Dkt Msonde.

Comments