CCM ARUSHA YATIKISA ELIMU YA UWEKEZAJI WA BANDARI, CHONGOLO AAPA HATA MBINGU ZIBINUKE HAWATA WAACHA DP WORLD KUWEKEZA NCHINI

WANAO POTOSHA MKATABA HUU UTAKUJA KUWASHANGAZA HAWATA AMINI MAFANIKIO MAKUBWA TUTAKAYO FIKIA KIUCHUMI.

Na Lucas Myovela - Arusha, Kusini mwa Tanzania.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo,amewataka watanzania kuto kuwa na hofu kwenye suala la uwekezaji la bandari ya Dar Es Salaam kwani matokeo yake yana tija kubwa ambayo itaonekana baadaye na kuwashangaza wanao beza uwekezaji huo.

Aidha Chongolo amesema upotoshwaji katika suala la bandari ni vita ya kiuchumi ambayo haiwezi kushikwa wala kuonekana kwa macho na Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye fursa nyingi za kiuchumi na kuwa ni vema kupima maneno ya upotoshaji.


Akizungumza katika Mkutano wa hadhara wa kutoa elimu ya makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uendeshaji wa bandari,ulioshirikisha wananchi kutoka mikoa ya Arusha,Kilimanjaro na Manyara.

"Nasi tunapenda kupendwa na wananchi hatuwezi kufanya jambo lisilo na tija kwa taifa,tuvute subira matokeo yake tutayaona na tuachane na upotoshaji unaoendelea ni vizuri kila mmoja akatambua hii ni vita ya kiuchumi hakuna anayetutakia jema la nchi yetu,"alisema


Aidha alisema kutokana na miradi mbalimbali inayoendelea nchini,kunahitajika fedha nyingi na moja ya upatikanaji wa fedha hizo ni kwenye uwekezaji kwenye bandari.

"Hata kwenye suala la utengenezaji wa filamu ya The Royal Tour watu wengi walibeza lakini leo tunaona matunda yake kufurika kwa watalii kwenye vivutuo vyeetu mbalimbali na watu wanapata matunda ya filamu hii hatumkumbuki wala kumshukuru tena Rais Dk Samia Suluhu Hassan,na matokeo yake tunakuja na lingine hatutendi haki,"aliongeza


Aidha alisema kama kwenye utengenezaji wa filamu hiyo Rais alipata maono ya kuongezea mapato zaidi hata kwenye suala la uwekezaji wa bandari nako matokeo yake yatakuwa chanya.

Katibu huyo alikemea baadhi ya watu wanaomtukana Rais badala yake waje na hoja za kusaidia serikali kuboresha makubaliano hayo kwa faida ya taifa.


"Tunakaribisha maoni ya watu juu ya suala hili lakini yote ya dharau,kebehi na matusi hatutayapokea na badala yake tutasonga mbele na mwisho wa siku watakuja kuishukuri serikali kwa maendeleo makubwa tutakayoyafikia,"

Aidha alisema kazi ya kuongoza nchi siyo lelemama inataka ukae imara na kusimamia mipango yako unayoiamini bila kuyumba au kuingia kwenye mitego ya wasioitakia mema taifa.


"Ukiona adui yako anakupigia makofi katika jambo lako achana nalo halina tija,ukiona adui anakupigia kelele kaza buti nenda mbele kwa sababu wanajua ukilitekeleza kwa kiwango hicho watakosa kupata dhamana mwaka 2025,nasi tunapenda kupendwa,"alisema na kuongeza


"Mpango unaoendelea sasa wa uwekezaji ni utekelezaji wa ilani ya CCM,wapo wanaohangaika kutupiga breki ili tusiendelee na utekelezaji huu na baadhi yetu wanaingia katika mtego wa kuanza kubishana,mtu asiyekupenda hawezi kukushauri jambo lenye tija,"alisema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof.Kitila Mkumbo, alisema katika uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam, utafanywa na wafanyabiashara, wakati serikali ikibaki katika jukumu lake la msingi la ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi.

"Kuwepo kwa bandari ni upendeleo wa kijiografia tuliobahatika kuwa na bandari sio nchi zote zimebarikiwa,lakini ni jukumu letu sisi binadamu kutengenezea miundombinu ili ziwe na faida za kiuchumi na tumekua tukizitengeneza mara kwa mara, lakini bado ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ni mdogo.

"Tunahitaji uwekezaji mkubwa pamoja na kuboresha utendaji, ili tupanue magati yetu, kwa ajili ya kuhudumia mizigo mingi zaidi,"alisema.

Prof.Kitila alisema katika uwekezaji huo,Mwekezaji huyo amepewa eneo la hekta 7.5 sawa na asilimia 8 ya eneo la bandari lenye ukubwa wa hekta 667.

"Serikali tumepokea maoni ya wananchi yenye tija na yasiyo na tija, kuhusu uwekezaji huu wa bandari na tutayachambua, kwa ajili ya kutusaidia kwenye mikataba ijayo,"alisema.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakidete alisema, sababu kubwa ya kutafuta mwekezaji kwa bandari hiyo ni, baada ya kuona meli nyingi za mizigo zinasimama muda mrefu kusubiri kushusha mizigo kwa ukosefu wa vifaa vya kutosha vya kushusha mizigo.

Alisema meli ya mizigo inaposimama inasubiri kwa siku tano hadi 15 na kusababisha gharama kubwa kwa mwenye meli, kulipa kwa siku ambazo anasubiri kushusha mzigo.

"Kwa siku tano gharama ya kusubiri kushusha mzigo ni dola 25,000 sawa na Sh.milioni 58 na ikisimama zaidi ya siku hizi na gharama yake inapanda juu zaidi ya hapo,"alisema.

Vile vile,sababu inayowasukuma kuwekeza ni za ushindani kutokana na sasa baadhi ya nchi za Uganda,Jamuhuri ya Congo,Rwanda,Zambia na Malawi kupunguza kushusha mizigo yao kwa bandari hiyo, kutokana na kukaa siku nyingi bandarini na kwenda nchi zingine kupitishia mizigo yao.

Alisema kwa sasa uwezo wa mapato kwa bandari hiyo ni Sh.Trilioni 7.76 ila watakapowekeza wataongeza mapato hadi Sh.Trilioni 26, ambayo yatatumika kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini.

"Kwa sasa serikali inapoteza mapato mengi katika bandari ya Dar es Salaam, kutokana na mifumo ya Tehama kutosomana,lakini mwekezaji wa DP World ataimarisha mifumo hiyo, pamoja na kuongeza uwezo wa Gati namba sifuri la kupokelea magari laki mbili na nusu kwa mwaka hadi milioni tatu,"alisema.

Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Steven Wasira, alisema wanaompinga Rais katika suala la bandari ni wale wanaomezea mate kiti cha urais wa mwaka 2025, wakidhani Rais Samia Suluhu Hassan angeshindwa kuongoza nchi ndani ya kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja pale alipokalia kiti hicho, lakini amewapiga bao.


"Hatuwezi kuuza uhuru wa nchi yetu sisi ndio tumeleta uhuru wa nchi hii,kwa hiyo hatuwezi kutishwa na vibaraka wa mabeberu, wanaosema nchi imeuzwa na bandari imeuzwa, huu ni uwongo.CCM imerithi mikoba ya kuongoza nchi hii, kutoka chama cha TANU na Afro Shiraz Party,"alisema.


Pia, alisema kinachowauma wapinzani ni Rais Samia kutekeleza miradi ya maendeleo, katika sekta mbalimbali pamoja na kuongeza bajeti ya kilimo na mifugo, kwa ajili ya kukuza uchumi wa wananchi wanyonge na mafanikio hayo, yamekuwa mengi kuliko uwongo wao.

"Sisi ni watanzania na Tanzania tumeiunda wenyewe hao wanaosema mambo ya Tanganyika ni watumwa wa mawazo,wanadai nchi imeuzwa kama kweli imeuzwa wao walikuwa wamekaa wapi?"alihoji huku akishangiliwa na wanachama

Alisema mipaka ya bandari italindwa na majeshi kama mipaka ya anga inavyolindwa na nchi kavu, hivyo hakuna sababu ya kusikiliza upotoshaji huo.


"Hawa wapinzani wanasubiri CCM tujikwae, lakini hatuwezi kujikwaa watabaki kama fisi, anayevizia mkono wa mtu uanguke, ili apate kitoweo,ila tumewapiga bao,"alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Uwekezaji na Mitaji Jerry Slaa, alisema mpaka sasa hakuna mradi wowote unaoendelea, kuhusu uwekezaji wa bandari hadi mikataba mingine miwili itakaposainiwa.


Alisema uwekezaji huo ufafanyika hatua kwa hatua, kwa kuzingatia sheria za nchi na maslahi mapana ya Taifa na hautajumuisha uwekezaji katika bandari ya Tanga na Mtwara pamoja na sekta ya ardhi.

 

"Baada ya mikataba yote kusainiwa iwapo mwekezaji huyu wa DP World atashindwa kufanya uendelezaji wowote, katika eneo la bandari lililo ndani ya mkataba kwa kipindi cha miezi 12 mkataba wake utakoma,"alisema.


Aidha, alisema hakuna eneo lolote la bandari lililouzwa na mkataba upo wazi, katika maeneo yatakayojikita kwenye uwekezaji huo, ambayo ni Gati namba sifuri, moja hadi nne,tano hadi saba.

Alitaja maeneo mengine yatakayohusika katika mkataba huo, ni ya mifumo ya Tehama,utoaji wa elimu na huduma za Meli zenye hadhi za kimataifa.

"Maeneo ya majahazi,maeneo ya abiria,Gati namba nane hadi 11 pamoja na Gati la mafuta hazipo katika uwekezaji wa DP World, hii inaamna kwamba siyo maeneo yote ya bandari hii ipo kwenye uwekezaji kama baadhi ya watu wanavyopotosha,"alisema


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM(UVCCM) Taifa,Mohamed Kawaida,amemuomba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kushughulikia wanaomtukana Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.


"Kwa niaba ya vijana leo nataka nitume salamu,vijana wa CCM kama kuvumilia tumeshavumilia sana na kama kuchoka tayari tumechoka,tunamtaka msajili wa vyama vya siasa awachukulie hatua,"alisema.


"Tumechoka na matusi anayotukanwa kiongozi wetu,awachukulie hatua.N kama hiyo haitoshi vijana tutamlinda Rais wetu,lazima tuwakemee hawa majizi wanaojaribu kukwamisha mradi huu,"alisema.


Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini,Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongela,alisema yapo mengi yanayozungumzwa, ila wanaamini mkakati wa serikali kuingeza mapato utaongeza nafuu kwa wananchi.


"Kanda ya Kaskazini tuna miradi mingi ya maendeleo inaendelea, sisi tuahidi miradi inasimamiwa tutahakikisha kuna ufanisi na kuondoa kero kwa wananchi,kuna mambo yanasemwa lakini sisi tunaamini kila mkakati wa serikali, kuongeza mapato tunaamini utaleta nafuu kwa wananchi," alisema Mongela.

Comments