FCF YAKABIDHI KITUO KIPYA CHA ASKARI ILI KUPAMBANA NA MAJANGILI NA TEMBO WAHARIBIFU

FCF yaikabidhi TAWA kituo cha askari kupambana na majangili na Tembo waharibifu.

Mwandishi wetu.

Taasisi ya uhifadhi ya Friedkin Conservation Fund(FCF) kwa kushirikiana na Kampuni ya Tanzania Game Tracker Safaris imekabidhi Mamlaka ya usimamizi wanyamapori nchini (TAWA) jengo la kituo cha askari wanyamapori ili kukabiliana na Ujangili na Wanyamapori waharibifu.

Kituo hicho kimejenjwa kwa gharama y ash 129.9 milioni katika kijiji cha Ng’hanga kilichopo jirani na pori la akiba la Maswa, wilayani Meatu mkoa wa Simiyu.

Katibu Tawala wa wilaya ya Meatu, Eliasa Mtalawanje ndio alikabidhiwa kituo hicho akiwakilisha mkuu wa wilaya hiyo, Fauzia Ngatumbura na baadaye alikabidhi funguo kwa TAWA.


Mtalawanje alipongeza taasisi ya Friedkin kwa msaada huo mkubwa ambao alieleza ni utekeleza wa Maelekezo ya Rais Samia Suluhu kumaliza migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu.

Alisema jvijiji vinavyozunguka Pori la akiba la Maswa, vimekuwa vikikabiliwa na changamato ya wanyama wakali na waharibifu kama Tembo hivyo, kujengwa kituo hicho kutapunguza migogoro hiyo.


Aliwataka askari wa TAWA ambao watakuwa katika kituo hiki kushirikiana na viongozi wa serikali katika eneo hili ili kukabiliana na ujangili.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Afisa Uhusiano wa FCT katika eneo la Mwangudo, Mulisu Richard alisema Jengo lakituo hicho lenye vyumba vinne, Ofisi na Jiko, pia wamejenga miundombinu ya uvunaji maji ya mvua na miundombinu ya umeme wa jua ambavyo vimegharimu sh 10.5 milioni.


Mulisu alisema, lengo la mradi huo ni kuimarisha ulinzi wa wanyamapori na kuwaweka askari karibu na jamii ili kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.


Akizungumza baada ya kupewa funguo za jingo hilo,Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa TAWA Kanda ya Ziwa, Said Kapanda alishukuru wawekezaji hao kwa kujenga kituo hicho.

Kapanda alisema kitasaidia sana kudhibiti wanyama kuvamia makazi ya watu na ujangili, kwani awali Askari walikuwa wakiishi mbali na eneo hilo.


“Tunawapongeza Friedkin na TGTS kwa msaada huu ambao utasaidia sana katika uhifadhi wa eneo hili”alisema


Meneja wa Maendeleo ya jamii wa FCF Tanzania, Aurelia Mtui alisema wataendelea kutekeleza miradi mbali mbali ili kusaidia jitihada za uhifadhi nchini.


“Tumekuwa na miradi ya kufanya doria za anga kwa kushirikiana na TAWA kila mwezi,lakini pia kufunga vifaa vya kusoma mawimbi kwa Tembo na Faru kwa kushirikiana na TAWIRI”alisema.


Kampuni ya TGTS imewekeza shughuli za uhifadhi katika pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu.

Comments