KAULI 3 TATA ZA ASKOFU BENSON BAGONZA ATUPA JIWE GIZANI ATOA ANDIKO AMBALO NI KITENDAWILI HADI SASA NA GUMZO KUBWA MITANDAONI.
ATOA MFANO WA AGANO LA KALE NA AGANO JIPYA.
AHOJI KKKT KAMA NI AGANO JIPYA AU LA KALE....?
Anaandika Askofu Dr.Benson Bagonza (PhD), Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe.
Wapendwa, nimejizuia sana kuandika au kusema chochote, lakini mmenisonga sana, mkitaka niseme neno. Nipo safarini kuelekea Vienna, Austria. Na kwa kuwa sijui kama nitafika niendako kabla hamjakata tamaa ya kunisikiliza.
Basi naomba niseme mambo haya matatu na myasome kwa furaha.
1. Tumetazamwa na dunia nzima kwa siku nne (tukiwa kwenye mkutano mkuu wa KKKT pale Arusha). Mtu mmoja ambaye ni mara ya kwanza kushiriki mkutano huo, alipoona yaliyotokea aliniuliza:
“Hivi nyie wenzetu Wachungaji na Maaskofu mmeshagundua kwamba mbingu haipo mkafanya iwe siri yenu tu?” Akaongeza, “kama mbingu ipo kwanini mfanyiane mabaya hivi? Tena hadharani?".
2. Nilizoeshwa kuamini kuwa watu wanakataliwa kwa sababu ya ubaya wao na wengine hupendwa kwasababu ya wema wao.
Lakini sasa nimeamini wapo wanaoweza kukataliwa kwa sababu ya wema wao na wengine wakapendwa kwa sababu ya ubaya wao. Kikubwa nilichojifunza ni kuwa ubaya hauwezi kukaa kwa amani na wema.
Tumefundishwa, katika Agano la Kale, kwamba kichafu kikigusana na kitakatifu kile kitakatifu kinaharibika (kunajisika). Lakini katika Katika Agano Jipya, kichafu kikigusana na kitakatifu, kile kichafu kinatakasika.
Je KKKT ni ya Agano Jipya au la Kale?.
3. Watu wakatili na waovu hujiandaa kupiga na kuangamiza wabaya wao wakati wote.
Watu wema hutafuta kuushinda ubaya kwa wema wakati wote. Kuna wakati wapigaji wakishapiga, huketi na kufurahi kuwa wamepiga.
Lakini wakitulia hugundua kuwa kumbe wao ndio wamepigwa sana.
Nimesamehe yote. Kutosamehe ni sawa na kunywa sumu ukitegemea afe adui yako.
Sumu uliyokunywa bila kukusudia inaua vibaya kuliko uliyokunywa kwa kukusudia.
Huku kwetu huwa HATUGOMBEI bali TUNAGOMBEZWA na kuzodolewa. Amani ya Kristo iwe nawe. Unione nitakapokuona (Tuonane).!.
Comments
Post a Comment