MALAIGWANANI WACHUTAMA SAKATA LA KUSHAMBULIWA WAANDISHI WA HABARI.

WAGOMA KUBURUZWA NA WACHACHE KWA MASILAHI YAO BINAFSI ILI KUWAGOMBANISHA NA SERIKALI KISA WAMERIDHI KUHAMA.

WAMUOMBA RAIS SAMIA KUENDELEA NA NIA YAKE NJEMA YA KUWAHAMISHA NA WAO WAKO TAYARI KUHAMA.

Na Lucas Myovela_Ngorongoro


Viongozi wa Kimila wa Jamii ya Kimasai Maarufu kama Malaigwanani wamesikitishwa na kulaani vikali kitendo kilichofanywa na wakazi wa jamii hiyo cha kuwapiga waandishi wa habari waliyokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kazi katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Mkoani Arusha.

Malaigwanani wameyasema hayoAgosti, 28,2023 katika Kijiji Nayobi kata ya Kapenjiro Wilayani Ngorongoro na kwa kueleza kuwa waliofanya tukio hilo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria bila kuonewa haya kwani wanawachonganisha Wamasai walio tayari kuhama kwa hiari yao na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan.

Wakiongea na Waandishi wa habari Mmoja wa Laigwanani hao wa kimasai ambae ni mkazi wa Nayobi Ngorongoro aliyejitambulisha kwa jina la Ikoyo Roinge, katika Mkutano wa Milla ya upatanisho ambao ulikuwa na lengo la kulaani na kukemeaa kitendo hicho cha kupigwa kwa waandishi wa habari na kusema kitendo hicho hakitarudiwa tena kwa kuwa wananchi walio ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wako tayari kuhama kwa hiari yao wenyewe.

‘’Tunalaani kitendo kilichotokea agosti 15, 2023, cha kupigwa waandishi wa Habari wakiwa na mkalimani wao na tunalaani sana jambo hilo lisitokee tena kwa sababu wamepigwa na kujeruhiwa waandishi hao bila hatia yoyote’’. alisema Roinge.


"Ndio maana leo tunafanya zoezi la upatanisho kwa wazee wote,wamama,viongozi wa Milla na jamii kwa ujumla kwa kuwa uhamisho ni jambo la hiari na sio vinginevyo’’ aliongeza Roinge.


Kwa upande wake Kiongozi Dini ya Roman Catholic (RC) kutoka katika Parokia ya Nainokanoka, Katekista Edward Leyani alisema wanawaombea msamaha wale wote waliohusika na tukio hilo kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndio mpatanishi wa kila jambo na huwa hapendi uvunjifu wa amani katika eneo lolote kwani wote ni Watu wake.


Leyani alieleza kwamba wale wote waliokuwa tayari walifanya maamuzi yao kwa hiari yao na wale wote wanaodai kuwa kuna watu wanawalazimisha wananchi wa Ngorongoro kuhama hiyo sio kweli kwani wanafanya hivyo kwa masilahi yao.

"Wananchi wa jamii ya kimasai wako tayari kuhama na kutii maagizo ya serikali inayoongozwa na Rais Samia na  hatutakubali kurubuniwa na mtu yeyote, kikundi kwa maslahi yao kwani maamuzi ya kuhama ni yao wenyewe na sio kulazimishwa". alisema Leyani.


Nae Laigwanani Ndwala Ndoishie akisoma Tamko la jamii ya Kifugaji ya Kimasai alisema wamefanya Milla kwa kuchinja Ng’ombe watatu,Ng’ombe mmoja kwa kumwaga damu ya kuomba radhi kwa uongozi wa NCAA,Ng’ombe wa pili kuomba radhi kwa serikali na Ng’ombe wa tatu kuomba radhi kwa Rais kufuatia tukio hilo.


‘’Kwa umoja wetu wamasai na wananchi wote tuishio ndani ya hifadhi ya  Ngorongoro, tunatoa tamko la utii kwa mama juu ya nia njema  yake ya kututaka  kuhama kwa hiyari kwamba tumepokea neno hilo kwa moyo mmoja na kwa Pamoja tunasema tuko tayari kuhama’’ Alisema Laigwanani Ndoishie.


Aidha laigwanani huyo katika tamko lake alisema kuwa serikali iwachukulie hatua kali za kisheria  wale wote wanaopotosha na kujaribu kukwamisha  zoezi hilo kwa maslahi yao binafsi  na kuchonganisha na serikali yenye dhamira njema kwa  wamasai wa Ngorongoro.


"Rais sisi Wamasai tunawafahamu wapotoshaji hao wakiwemo  wanasiasa, wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, wanaharakati, Asasi za Kiraia na Jumuiya za Nje ambao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kutulaghai na kutufanya mitaji yao hali inayopelekea  kutufanya tuendelee kuwa masikini zaidi wakati wao na familia zao wanaishi nje ya hifadhi ya Ngorongoro,na sisi kutufanya tuendelee kuwa watumwa wao na sasa tunasema imetosha’’. sehemu ya tamko hilo

Viongozi hao wa Milla walimwomba Rais kuendeleee kusimama imara, bila kutetereshwa,kuyumbishwa na maneno ya wapotoshaji kwa wao wapo tayari kuhama muda wowote bila kusukumwa.





Comments