MHE. ZUBEIR AIPONGEZA NACTVET.
Na Mwandishi Wetu.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, ameipongeza NACTVET kwa kushiriki maonesho ya 4 ya Elimu ya Juu yanayoendelea Zanzibar na kusisitiza NACTVET iendelee kutoa taarifa zenye tija katika masuala ya Elimu. Aidha, amehimiza utoaji elimu zaidi juu ya miongozo na taratibu za kujiunga na Vyuo wakati wa maonesho hayo ambayo ni fursa nzuri ya kukutuna na wadau.
Mhe. Zubeir ametoa pongezi hizo leo 31 Agosti,2023 alipotembelea banda la NACTVET akiwa ni mgeni rasmi katika ufunguzi rasmi wa Maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Maisara Zanzibar.
Akiwa katika banda la NACTVET, Mhe. Zuberi amepatiwa maelezo na Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora NACTVET, Dkt. Jofrey Oleke kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa NACTVET Dkt.Adolf Rutayuga, kuhusu majukumu ya NACTVET na inavyoshirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika kusaidia kuendesha vyuo vya kati vilivyopo kisiwani humo.
Aidha, Dkt. Oleke ameongeza kusema kuwa kwa upande wa Zanzibar NACTVET inasimamia Vyuo 17 vinavyotoa kada mbalimbali hivyo bado NACTVET ina jukumu kubwa la kuwafikia wadau zaidi kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusiana na ujuzi.
Miongoni mwa wageni alioambatana nao Mgeni Rasmi ni pamoja Naibu Waziri, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Ali Abdul Gulam na Katibu Mkuu ,Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali, Mhe. Khamis Abdalla.
Comments
Post a Comment