RAIS SAMIA: UPOLE SIYO UJINGA NA KUMISHWA WIZARA SIYO ADHABU.

MLITAKA UTAMU WA NGOMA SASA INGIENI MCHEZE MJIONEE. 

DKT MPANGO ASEMA RAIS SAMIA ANAPANGA SAFU YAKE YA USHINDI.

Na Lucas Myovela_ Motive Tv.


Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaapisha Viongozi wateule Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo September 01,2023 ambapo amesema mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu aliyoyafanya sio adhabu bali ni mabadiliko ya kawaida ya kuimarisha maeneo ya utendaji kazi.

“Mlipoanza kuapa mmesema ‘Mimi fulani fulani naahidi umma kwamba nitakuwa Mzalendo n.k’, sasa kile kiapo mnaweza kuona mmeapa tu kwasababu Jaji Mwangesi anataka muape, hapana, ni kiapo ambacho hata Mungu anakisikia naomba mkatimize kiapo chenu”.Amesema Rais Samia.


“Mabadiliko haya ni adjustment , maendeleo lazima yawe na bandika bandua, kaza nati fungua, toa nati hii weka hapa ndio maana ya mabadiliko haya lakini tukikaa wenyewe (Kwenye kikao kazi) nitawaeleza kiundani”. Amesema Rais Samia.


“Kwa wale wapya Jerry Silaa na wengine nadhani mnayaona yanayotokea Bungeni na mmekuwa mkipaza sauti kubwa kwa Mawaziri sasa yale mliyokuwa mnapaza kwa Mawaziri mnakwenda kuyafanya nyinyi, wanasema ukitaka uhondo wa ngoma…? sasa mpo kwenye ngoma tunatarajia mcheze kwelikweli na mlete yale mabadiliko mliyokuwa mkiyahoji”.Ameongeza Rais Samia.


“Mabadiliko haya sio adhabu, ni mabadiliko ya kawaida ya kuimarisha maeneo yetu, natarajia commitment na utumishi, sisi ni Watumishi wa Watu sasa kuna mwingine akipata uteuzi anajiona eeh atanijua Mimi ni nani, sisi ni Watumishi wa Watu, katika utumishi mahusiano ni jambo zuri sana, ukijipandisha unataka kukaribia Mbinguni kwamba umepata uteuzi wewe nani wewe nani hutotumikia Watu”. Amesisitiza Rais Samia.


UPOLE SIO UJINGA.


Aidha Rais Samia amesema ameeleza kuwa kwa wale wanao dhani upole ni unjinga sivyo hivyo ila bali upole unaweza kukufanya ukafanya kazi kwa ufanisi na umakini wa hali ya juu maana utatoa maamuzi yenye tija kwa sababu utakuwa umepata muda mwingi wa kutafakari jambo husika.


 “Upole sio ujinga hata kidogo, upole sio ujinga, upole saa nyingine ndio maarifa, unatulia unafikiri jambo mara mbili mara tatu kabla hujatoa kauli naomba Viongozi mkatulie mtumikie Watu”. Amesema Rais Samia.


“Lingine la tatu amelisema vizuri sana Makamu wa Rais ni reform, tunachotaka ni mabadiliko tunayowaahidi Watu, tunaahidi mambo mengi twendeni tubadilikeni , nitawaambia Mabingwa wa reform mmoja nimseme hapa Mchengerwa kwa mfano, nilimpopeleka Utumishi mwanzo namteua kaingia na kasi papaa papaa papaa kelele zikawa nyingi, nikasema mmh labda Waziri wangu nae kazidi kapandisha mabega, mpeleke Wizara ya Michezo, kaenda michezo kazi aliyoifanya mmeiona kaacha kazi nzuri sana”. Ameongeza Rais Samia.

“Nimempeleka Wizara ya Utalii mipango aliyoiweka, Angellah Kairuki ukienda kufuata mipango aliyoweka Utalii inakwenda kupanda, Dr. Hassan Abbas (Katibu Mkuu) yuko pale mzuri sana ameweka mipango mizuri pale na Waziri kwako ni kusimamia utendaji yatekelezwe yaliyowekwa tupandishe Sekta, sasa Mchengerwa nimempeleka TAMISEMI mwakani kuna kivumbi na Mimi nakujua najua unaweza, kivumbi kile kinakufaa na kifua chako najua unaweza kwahiyo nimekupeleka TAMISEMI ni kazikazi”. Amesisitiza Rais Samia.


DKT MPANGO: RAIS SAMIA ANAPANGA SAFU YA USHINDI.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona ni vema apange safu ya ushindi ambayo inaweza kufunga magoli zaidi ili kuanzia mwakani Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2025 Uchaguzi Mkuu yakafungwe magoli ya uhakika sio ya kubabaisha.


Akiongea mbele ya Rais Samia wakati wa kuwaapisha Viongozi Wateule Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo Sept 01,2023, Dkt. Mpango amesema “Nawapongeza Wateule wote katika nafasi mbalimbali, kama ambavyo Kocha yoyote anafanya Mh. Rais imempendeza amewaamini amebadilisha namba zenu za kucheza mpira, maana Mawaziri karibu wote sura zilezile lakini tumebadilisha nafasi na tukiacha mmoja na Manaibu Mawaziri tukiacha wachache”

“Nawaomba sana, Mh. Rais anataka tija zaidi katika utendaji kwahiyo muende mkashirikiane, mzingatie falsafa ya Mh.Rais ya zile R nne, nami natilia mkazo ile ya kusimamia mabadiliko (Reforms)”


“Mmemsikia Makamu Mwenyekiti (Mzee Kinana), ni muhimu sana muwe na masikio juu ya kero za Wananchi wetu Bara na Visiwani na kuzifanyia kazi, yapo maeneo kelele ni kubwa kila unapokwenda, nikimuangalia Jerry Silaa kwenye ardhi kero kubwa ukaongoze timu yako kuhakikisha kero upande wa ardhi zinashughulikiwa ipasavyo, pia upande wa Maliasili magomvi kati ya Wananchi na Hifadhi zetu ni makubwa Waziri ukashirikiane na mwenzako wa mifugo tunapoteza Watu n.k”. 


“Mheshimiwa Rais ameona ni vema apange safu ambayo inaweza kufunga magoli zaidi ili twende kuanzia mwakani Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2025 Uchaguzi Mkuu twende tukafunge magoli ya uhakika sio ya kubabaisha”. amesema Dkt Mpango.

Comments