NAIBU WAZIRI MKUU DKT, BITEKO AWATAKA VIONGOZI WAKUBWA KWAUNGA MKONO WAKU WA WILAYA WABUNIFU.

Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko amewataka Viongozi wakubwa Serikalini kuwaunga mkono Wakuu wa Wilaya wanaobuni na kuja na ubunifu na kuwataka wawaone ni wenzao na wala sio Washindani wa mawazo ambapo amesema ipo changamoto inayochelewesha mambo ya kwamba pale Kiongozi Mdogo (Mfano DC) akibuni kitu, basi Mkubwa wake huona kama amemuwahi  jambo alilopaswa kufanya yeye na hivyo kuanza kumuwekea ugumu. 


Dkt, Biteko amesema “Kama Wilaya zote zingekuwa na ubunifu wa kufanya matukio ndani ya Wilaya hizo, imani yangu Wizara nazo zingepunguziwa mzigo wa kufikiri kwa niaba ya Wilaya, nitoe wito Sisi tuliomo Serikalini, Wilaya zinazobuni na kuja na ubunifu wa aina hii tuwaunge mkono, tuwaone ni wenzetu na wala sio Washindani wa mawazo”.


“Kwasababu ipo changamoto akiwaza Mdogo, Mkubwa anaona umeni-time ili jambo nilipaswa kufanya Mimi, kufanya hivyo tunachelewesha, ni lazima wote tufikiri kuona tunasukuma mbele ndoto ya Mheshimiwa Rais, ili Mheshimiwa Rais afikiri mambo makubwa, madogomadogo akishuka akute sisi tumeshayamaliza kwasababu tuna ushirikiano mkubwa” 


Biteko amesema hayo wakati wa Pangani Investment Forum inayolenga kuifungua Pangani kiuwekezaji ambayo imefanyika usiku wa kuamkia leo kwenye Swahili International Expo 2023 Jijini Dar es salaam ambapo kupitia forum hiyo Biteko amezindua Filamu ya Pangani Royal Tour na  amekabidhi pia hati ya udhamini ya Dkt Samia Suluhu Tourism Scholarship 2023 kwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt Florian Mtey, udhamini huo utawasaidia Wanafunzi 20 kutoka Wilaya ya Pangani kujiunga na Chuo cha Taifa Cha Utalii ikiwa ni jitihada za DC wa Pangani, Zainab Abdallah kuwasidia Vijana wa Panga kujipatia elimu ya Utalii ili wahudumie Watalii wanaofika katika fukwe na vivutio vingine vya Pangani kwa weledi na viwango vya kimataifa. 


Biteko amezindua pia Pangani Investement Guide ambacho ni kitabu cha mwongozo unaoelezea  fursa zote za uwekezaji zilizopo Pangani na amegawa tuzo kwa waliofanikisha uwekezaji Pangani wakiwemo Clouds Media Group.

Comments