WATAALAM WA AFYA YA BINADAMU NA MIFUGO KUSHIRIKIANA KUDHIBITI ONGEZEKO LA VIMELEA NA MATUMIZI MABAYA YA DAWA
Na Lucas Myovela.
Waziri wa mifugo na uvuvi Mhe, Abdallah Ulega amewataka wataalamu wa Afya ya binadamu na mifugo kushirikiana kudhibiti ongezeko la usugu wa vimelea na matumizi mabaya ya dawa.
Amesema hayo Jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kongamano la tatu la kitaifa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa za binadamu na wanyama.
Mhe, Ulega amesema asilimia 70 ya magonjwa ya binadamu yanatokana na wanyama hivyo Kuna ulazima wa kujenga ushirikiano wa pamoja kati ya wataalamu wa Afya wa magonjwa ya binadamu na Wanyama ili waweze kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
"Ongezeko la watu Duniani limepelekea kuwa na mahitaji makubwa ya chakula na dawa na hivyo kupelekea watu kutaka kuchukua dawa bila kuwa na cheti cha daktari na hivyo kupelekea usugu wa dawa kwa magonjwa ya binadamu". amesema Mhe, Ulega.
Awali mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela aliwapongeza wataalamu wa Afya kwa kuelimisha uma juu ya madhara ya kutumia dawa bila cheti cha daktari ili kupunguza usugu wa dawa kwa magonjwa ya binadamu.
Amesema kuwa mfumo shirikishi kati ya wataalamu na watendaji wa Serikali ngazi ya Mkoa mpaka kijiji utasaidia sana kupunguza usugu wa dawa.
Mkurugenzi wa mifugo nchini Profesa Hezron Nonga akizungumza katika kongamano hilo amesema muongozo wa matibabu ya wanyama utawasaidia wataalamu wa Afya za wanyama kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kwa wanyama kabla ya kuwatibu.
Amesema kwa sasa Kuna madaktari wa mifugo 1061, madaktari wasaidizi 4300 na wataalamu wa maabara 70 ambao wamesajiliwa na kutambuliwa.
Amesisistiza kuwa kongamano hilo litasaidia kuja na mkakati madhubuti wa kupunguza usugu wa vimelea sugu dhidi ya dawa za binadamu na mifugo
Comments
Post a Comment