HAYA NDIYO MAISHA NA SAFARI YA DKT NCHIMBI KATIKA ULIMWENGU WA SIASA. HADI KUWA KATIBU MKUU WA CCM TAIFA. NA HALI YA KISIASA ILIVYO NCHINI.

Na Lucas Myovela - Zanzibar.

DKT. EMMANUEL JOHN NCHIMBI ACHAGULIWA KUWA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI CCM.

Emmanuel John Nchimbi (aliyezaliwa 24 Desemba 1971) ni mwanasiasa Mtanzania wa CCM na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini tangu 2010. Alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

HISTORIA KAMILI YA DKT. NCHIMBI.

Dkt, Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya, (atafikisha miaka 53 Desemba mwaka huu). Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986.


Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.


Dk Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.


Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).


Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).


Dk Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.


Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).


Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.


Dkt, Nchimbi amemuoa Jane na wana watoto watatu.


MAISHA YA SIASA NA MBIO ZAKE ZA KUWANIA UBUNGE.

Dk Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu. Dk Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.


Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.


Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.


Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.


Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013.


 KUCHAGULIWA KWA DKT, NCHIMBI KUWA KATIBU MKUU WA CCM TAIFA.

Chama Cha Mapinduzi kupitia kikao cha Wajumbe wake wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa sauti moja wameridhia na kumpitisha Ndugu. Emmanuel John Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM - Taifa).


Kikao hicho kimeketi leo tarehe 15 Januari, 2024 Kisiwani Zanzibar kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Wa Tanzania Ndugu. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Dkt, Nchimbi anachua nafasi ya aliekuwa katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe, Chongolo kujiudhuru nafasi hiyo mwaka jana 2023 kwa lidhaa yake mwenyewe na kumuandikia barua ya wazi Mhe, Mwenyekiti wa chama hivho cha CCM Dkt, Samia Suluhu Hassan ya kumuomba aweze kukubali Chongolo kuachia nafasi hiyo. 


MWENEZI MAKONDA ATOA TAARIFA YA MREJESHO WA SEMINA YA MAFUNZO NA KIKAO CHA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndugu. Paul Makond akizungumza kwa kueleza yaliyojiri katika Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika mapema leo tarehe 15 Januari, 2024 Kisiwani Zanzibar kilochoendeshwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mwenezi Makonda ameeleza yaliyojiri katika Semina maalum ya Mafunzo kwa Wajumbe wa Halmshauri Kuu iliyofanyika siku ya tarehe 13 na 14 mwaka huu.


Katika Semina hiyo, Mwenezi Makonda amesema kuwa Wajumbe wamepata nafasi ya kushiriki kujua hatua zilizofikiwa katika Mradi wa Umeme wa Mwl. JK. Nyerere.


Pia, kujua hatua na kazi inayofanyika katika muendelezo wa Ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR.


Vilevile, kujua hatua na muendelezo wa utekelezaji wa Ujenzi wa Daraja la Magufuli (Kigongo - Busisi).

Pamoja na hayo, Wajumbe wamepata nafasi ya kujadili na kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa upande wa Zanzibar.


Mwenezi Makonda amebainisha kuwa kupitia Kikao hicho, Wajumbe wampokea taarifa za maandalizi katika kuelekeza Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024 na Maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za CCM kuelekea kufikisha miaka 47 mwezi februari mwaka huu.


Aidha, Mwenezi Makonda amesema Wajumbe wa Halmashauri Kuu kwa pamoja wamepokea jina kutoka kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa la atakayechukua kijiti cha nafasi ya Katibu Mkuu na kwa pamoja wameridhia kwa sauti moja ya kwamba Ndugu. Emmanuel John Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa.


Kwa upande wake waziri wa fedha Dkt, Mwigulu Nchemba kupitia ukurasa wake wa twita ( X ), Amesema chama hivho kimeweza kuongeza mpambanaji na mshambuliaji wa siasa safi ndani ya Chama hicho cha CCM.

"Tumeongeza Kiungo Mshambuliaji (Central Midfilder), Striker tunaye SSH2025, Playmaker tunaye Kiungo muungwana PMpango, Beki Mkoba tunaye Kinana, KiungowaUlinzi tunaye, HAMwinyi. Mimi naomba nipangwe Winga, hakika watalala na Viatu 2025. Tunasajili wao wanalalamikia REFA ATAKUWA NANI (Yaani Tume), OOH SHERIA ZIBADILISHWE (Sheria za Uchaguzi). 💪💪💪💪 HONGERA SANA DR NCHIMBI". Amesema Mwigulu.


Aidha pia viongezi wengine mbalimbali wa chama hicho wameendelea kumpongeza Dkt, Nchimbi kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo na huku wakieleza ni ufunuo mpya wa chama hicho.


Kuchaguliwa kwa Dkt, Nchimbi na vuguvugu la kisiasa.


Mwanaharakati huyo wa Kisiasa Dkt, Nchimbi leo Januari 15,2024 anachaguliwa kushika nafasi ya Katibu Mkuu ili Kukitumikia chama chake cha mapinduzi ( CCM ), huku hali ya kisiasa ikiwa imechangamka kupitia vyama vya upinzani ambapo chama kikuu cha upinzani cha Demokasia na Maendeleo ( CHADEMA ) kikiwa kimetangaza maandamano ya Amani nchi nzima kushinikiza marekebisho miswaada mbalimbali hasa yale ya tume ya uchaguzi.


Kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ) Taifa Ndg, Freman Mbowe, ambapo Januari 13,2024 alitangaza kupitia chama chake kufanya maandamano nchi nzima Januari 24, 2024 ili kushinikiza mabadiliko ya miswaada mbalimbali ambayo alisema inamnyima haki mtanzania. 

Aidha pia kupitia matamko ya viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa kati ya CCM na CHADEMA wamekuwa wakijadili swala zima la kufanyika MDAHALO kabla ya kufanyika maandamano hayo.



Comments