UKWELI WOTE WA VUGUVUGU LA MIRERANI: HAKUNA MGODI ULIYOFUNGIWA MIRERANI.

WAMILIKI WA MIGODI YA TANZANITE WASISITIZWA KUZINGATIA SHERIA ZA UCHMBAJI.


"MWEKEZAJI KITALU C ALIWAITA WOTE WALIYOTOBOZA KWENYE MGODI WAKE WAPO WALIYO KUBALIANA NA KAZI ZA UZALISHAJI ZINAENDELEA".

Na Lucas Myovela - Mirerani

Afisa Mfawidhi wa Madini Mirerani, Nchagwa Chacha Marwa amewataka wamiliki wa migodi ya Tanzanite Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kuheshimu mipaka ya leseni ya uchimbaji kama sheria inavyoelekeza na kueleza kuwa Serikali haijafunga mgodi wowote wa Tanzanite Mirerani.


Pia Marwa ameeleza kuwa Serikali haijawahi kumwonea mwekezaji yeyote wala kumnyanyasa mchimbaji wala mmiliki wa mgodi wa Tanzanite Mirerani bali Serikali inasisitiza wamiliki wa Migodi kuzingatia sheria ya leseni ya uchimbaji namba 6 ya mwaka 2010 inavyoelekeza na sio vinginevyo.

Marwa alisema hayo katika mahojiano maalumu ofisini kwake Mirerani na waandishi wa habari na kusema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inawalinda na kuwajali wachimbaji wadogo,wakati na wakubwa kwa sera za madini na sheria za madini zinavyo elekeza na wawekezaji nao wanapaswa kufuata sheria kama Serikali ilivyoelekeza.


"Sheria ya madini iko wazi juu ya mipaka ya uchimbaji wa madini ya Tanzanite ndani ya mgodi na sheria hiyo haiwezi kuondolewa ama kukiukwa kwa kulalamika katika vyombo vya habari na kama unaona kuna changamoto ofisi iko wazi na inaweza kutatua au kutoa mwongozo wa nini kifanyike". Alisema Marwa.


Akizungumzia mgogoro wa mgodi wa Sanninu Laizer maarufu kwa jina la Bilionea alisema, Mnamo mwezi Novemba 21 mwaka 2023 walikuwa wamiliki wa migoni minne na waliitwa ofisini kwake na kuelezwa kwa nini waliingia kitalu C kinyume na taratibu hivyo wanapaswa kurudi nyuma na baadhi yao walikubali kwa maandishi baada ya kukaa mezani na wamiliki wa Kitalu C.


"Tarehe 21, 11, 2023 tuliweza kufanya kikako na wamiliki wa migodi ya kitalu D ambao walitoboza kwenda kitalu C, baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wamiliki wa kitalu C kwamba kuna baadhi ya wachimbaji wametoboza katika mgodi wake, kweli kwenye kikao hicho wote walikubali kuwa walikiuka leseni yao na kuingia kitalu C".Ameeleza Marwa.


"Baada ya mongezi ya kina baina ya pande zote tulifika makubaliano kwamba ndani ya siku kumi na nne watakuwa wamerudi nyuma na kuwaeleza wakakubaliane kwanza na Wamiliki wa kitalu C na watakacho kubaliana walete maazimio ya pamoja ofisini kwangu ". Aliongeza Marwa.


"Kweli ilipofikia siku ya makubaliano wapo walioleta makubaliano yao kwa maandishi baina yao na wamiliki wa kitalu C na sisi kama wasimamizi tuliyapokea na kila mtu kubaki na nakala yake ya makubaliano na kwa kweli wamiliki wa kitalu C walionyesha nia ya ujamaa na uzalendo kwa wachimbaji wenzao kwa kuwakubalia hiyo migodi mitatu kati ya minne iliyotoboza kwao". Aliongeza Marwa.


"Toka mwezi disemba mwaka jana hadi leo hii Bilionea Laizer hajafanya hivyo pamoja na kuhitajika kufanya hivyo mara kwa mara na mimi mwenyewe nashangaa habari zinazo endeleo katika vyombo vya habari mbali mbali siwezi jua nini dhumuni lake au huenda amefuatwa na waandishi ila ukweli ni kwamba bado yeye anasubiliwa katika meza ya maridhiano na mgodi wake haujafungwa unaendelea na uzalishaji hadi sasa ila kilicho fungwa ni njia ya kwenda kitalu C sehemu ambayo siyo leseni yake ya uchimbaji". Alisistiza Marwa.

Aidha Marwa alisema kabla ya kikao hicho wote walioingia kitalu C njia zao zilifungwa kuelekea kitalu C lakini njia nyingine ndani ya mgodi shughuli za uchimbaji ziliendelea ikiwa ni pamoja na mgodi unaomilikiwa na Bilionea Laizer.


Migodi iliyokubaliana kurudi nyuma baada ya njia zao kufungwa kuingia Kitalu C ni pamoja na Mgodi wa Manga Gems,Tanzania Exprolore Gem ,Mgodi wa Edward Mollel maarufu kwa jina la Dunia na Mgodi wa Bilionea Laizer.


Afisa Mfawidhi wa madini Mirerani amemtaka Bilionea Laizer kutekeleza ahadi yake aliyoahidi ya kuwapeleka wataalamu wa mipaka kupima eneo ndani ya mgodi kama kweli aliingia kitalu C au la kwani ofisi ya serikali iko wazi na inamsubiri yeye kutekeleza hilo bila upendeleo wowote.

Kwa upande wao uongozi wa kitalu C wamesema mpaka sasa bado wanamsubikia Laizer kufanya kama walivyokubaliana katika vikao ili waendelee kushirikiana katika ujenzi wa Taifa kwa pamoja kama walivyo fanya wenzake na hawapo tayari kuona mitobizano haramu katika eneo lao la leseni.


"Ni kweli tulikaa kikao na hadi sasa watatu tumekubaliana nao ila bado Laizer na sisi hatujui kama mgodi wake umefungwa ila tulifunga njia za kuja mgodini kwetu kwa mujibu wa sheria ikiwa ni njia ya kukaa mezani pamoja tukubaliane nini cha kufanya ila hadi sasa hajafanya hivyo, Pia sisi bado tunamsubilia alete wataalamu wake wapime ili tujue ameingia umbali gani kwenye eneo letu la uchimbaji ili kwa pamoja tuone tunasaidiaje". Alisema Meneja wa Mgodi wa Kitalu C Bw, Vitus Ndakize.

Kwa upande wa mchimbaji wa madini ya Tanzanite Ndg, Saniniu Laizer akiongea kwa njia ya simu yeye alikiri kufungiwa njia kuingia kitalu Cna kusema kuwa hawezi kukaa meza ya maridhiano na mwekezaji aliyemfungia njia na suala jambo ameiachia serikali ndio yenye maamuzi juu ya mgodi wake.


"Ni kweli nimefungiwa njia ila sipo tayari kukaa katika makubaliano maana sioni haja ya kuendelea na jambo hilo, Nimeongea sana na waandishi wa habari ila wao wanaenda kuandika wanavyo jua, kwasasa naendekea na uchimbaji kwenye mgodi wangu kwa maana ninazo njia tatu". alisema Saniniu.

Mwisho



Comments