LESENI 2648 ZA MADINI KUFUTWA TZ.

WAOMBAJI WAPYA WENYE MITAJI KUPATA FURSA KUENDELEZA MAENEO HAYO.


Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, kufuta jumla ya maombi na leseni za utafiti 2648 ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuomba na kuendeleza maeneo hayo kwa manufaa ya Taifa na ukuzaji wa sekta ya madini.

Waziri Mavunde amesema kuwa kumekuwa na baadhi ya wamiliki wa leseni ambao wamekuwa hawazingatii utekelezaji wa majukumu yao ya umiliki wa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123.


Miongoni mwa makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ni pamoja na wamiliki wengi wa leseni kutoanza au kutoendeleza maeneo ya leseni zao na badala yake kuhodhi maeneo, kutolipa ada stahiki za leseni, kutowasilisha nyaraka muhimu kama mpango wa ushirikishwaji wa Watanzania kwenye shughuli za madini (Local Content Plan), mpango wa wajibu wa makampuni kwa jamii (Corporate Social Responsibility) na nyaraka za taarifa za fedha kuonesha matumizi yaliyofanyika pamoja na vielelezo vya matumizi husika.


"Ninatoa mfano kuna watu 6 tu wanahodhi maeneo yenye ukubwa wa ekari milioni 13 ukubwa wa maeneo hayo ni sawa na ukubwa mara nne wa mkoa wa Kilimanjaro na hayafanyiwi chochote ilihali mahitaji ya maeneo ya uchimbaji ni mkubwa sana hapa nchini na hasa kwa wachimbaji wadogo ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana kwenye kukuza sekta ya madini," amesema Mavunde.

Comments