SENSA YA WANYAMA TANZANIA YATIKISA KWA WINGI WA NYATI,TEMBO,SIMBA NA CHUI BARANI AFRIKA.

 SERIKALI YAPOKEA OMBI LA TAWIRI KUWEKA FEDHA KATIKA SENSA YA IKOLOJIA ZOTE 11 KWA MANUFAA YA UTALII WA NCHI.

MATOKEO YA SENSA KATIKA MIFUMO MITATU YA IKOLOJIA.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Angellah Kairuki ametangaza rasmi matokeo ya sensa ya wanyamapori katika mifumo mitatu ya ikolojia ya Nyerere-Selous-Mikumi, Saadani-Wamimbiki na Serengeti ambayo ni miongoni mwa mifumo 11 ya ikolojia, huku akizitaka  idara ya wanyamapori kuja na mpango mkakati wa kuongeza idadi ya Twiga na Sheshe, kutokana na wanyama hao kupungua idadi yake na hivyo kutishia kutoweka kwa wanyama hao nchini Tanzania.

Akitangaza matokeo hayo katika mkutano wa wadau wa uhifadhi na utalii uliofanyika jijini Arusha, Mhe. Kairuki amesema, sensa katika mfumo ikolojia wa Nyerere-Selous-Mikumi, unaonesha kuimarika kwa spishi 22 za wanyamapori wakiwemo nyati/buffaloes (59,878), tembo/elephants (20,006), nyumbu/wildebeest (19,060), kongoni/hartebeest (18,361), swalapala/impala (14,031), ngiri (13,806) na idadi ya Wanyama walioonekana kwa idadi ndogo ni twiga/giraffe (1,679), Tandala mkubwa/greater kudu (1,414) na puku/sheshe (496).


"katika mfumo huu kumekuwa na ongezeko la tembo 20,006 (2022) ikilinganishwa na sensa ya awali 15,501 (2018) na Viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa kutoka 16% mwaka 2018 hadi hadi 0.8% mwaka 2022" ameeleza Mhe.Kairuki.


Mhe.Kairuki ameitaka Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii kuchukua hatua za haraka kulinda idadi ya Sheshe/puku ambao wanapatikana Tanzania pekee waliosalia katika maeneo yao ya asili yakiwemo mapori ya akiba ya Kilombero na ziwa Rukwa ambao idadi yao imepungua kwa kiasi kikubwa kutoka (1,579 mwaka 2018) hadi (496 mwaka 2022).

Vilevile , uhesabuji wa Nyumbu katika mfumo ikolojia wa Serengeti 

Matokeo ya sensa hii yamebaini uwepo wa nyumbu wanapatao 1,597,850. Idadi hii inaonyesha kuimarika kwa nyumbu ikilinganishwa na sensa ya hapo awali (2015) iliyoonyesha uwepo wa nyumbu wapatao 1,326,709.


Kwa upande wa mfumo ikolojia wa Saadani - Wami - Mbiki Matokeo ya sensa yameonesha uwepo wa wanyamapori wachache unahusishwa na hali ya upya wa hifadhi hizi ambapo hapo awali,hifadhi ya Saadani ilikuwa pori tengefu na sehemu nyingine ilikuwa shamba la mifugo na zoezi la kuongeza wanyamapori lilifanyika miaka ya hivi karibuni .


Aidha ,Mhe. Kairuki amesema kwa mwaka wa fedha 2024-2025 wizara imeweka mikakati ya kufanya sensa ya wanyamapori katika mifumo yote ya ikolojia kwa lengo la kuimarisha uhifadhi na kukuza kuwa na utalii endelevu ambapo ametoa rai kwa wadau kuonga mkono jitihada hizi za Serekali katika kuhifadhi utajiri wa Maliasili ya Wanyamapori .


"Katika hili nahitaji kasi zaidi katika udhibiti wa shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya uhifadhi pamoja na kuhamasisha suala la utunzaji wa mazingira na kutokukata miti hovyo ili kuendelea kutunza mazingira kwa faida ya viumbehai". Amesema Kairuki.

Kwa upande mwingine Waziri Kairuki amesema kuwa Upande wa Zanzibar, Raia wa Ethiopia na Kenya waliongoza kwa kufika visiwani humo na Ripoti inaonesha kuwa Waliofika Zanzibar kwa wingi walikuwa wanandoa ama Wapenzi wakati kwa Tanzania bara wengi wakitajwa kutokuwa na mahusiano ya kindoa.










Comments