ALIYEKUWA MSAIDIZI WA RAIS SAMIA AAPISHWA KUWA DC.

MAGOTI AAPISHWA KUWA DC KISARAWE AAHAIDI MAZITO YA KIMAENDELEO.

Aliyekuwa Msaidizi wa Siasa wa Rais, Petro Magoti ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe huku akiahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wengine.

Juni 6, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko katika ofisi yake kwa kuwahamisha wasaidizi wake kadhaa akiwamo Magoti akichukua nafasi ya Fatma Nyangasa aliyehamishiwa Kondoa mkoani Dodoma.


Magoti amekula kiapo hicho mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge huku watumishi wengine wakishuhudia tukio hilo


Akizungumza baada ya kiapo hicho kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Kibaha, Magoti amesema kutokana na imani aliyopewa na Rais Samia, atahakikisha anaendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa huku akiwa mwepesi wa kupata ushauri.


"Hii nchi ina watu wengi na ni wasomi lakini Rais ameona anipe nafasi hii ili nije nisaidie kusukuma maendeleo ndani ya Mkoa wa Pwani kwa kipande cha ardhi ya Kisarawe, niseme nitafanyakazi kwa bidii," amesema Magoti.


Amesema kwenye utekelezaji wa majukumu kuna changamoto nyingi hasa kwa mtu mwenye nafasi ya uamuzi kwa kuwa wakati mwingine wapo ambao hawapendi kupata ushauri kutoka kwa watu wakihisi hatua hiyo inawashushia hadhi, jambo ambalo si kweli.


"Napenda sana ushauri na kuna watu wakiwa na nafasi ya madaraka huwa hawapendi ushauri wakihisi kuwa vanapopewa ushauri wanashushwa hadhi, hilo jambo siyo zuri," amesema Magoti.


Pia, amesema katika utendaji kazi hapendi kukaa kimya pale inapoona kuna mtu amekosea utekelezaji wa majukumu badala yake anapenda kuçhauri kwa mazungumzo ili kuzuia kosa lisijirudie.


kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe, Kunenge amesema anaamini atafanyakazi kwa ushirikiano na watendaji wengine ili kuendeleza gurudumu la maendeleo.


"Hapa Pwani tunafanya kazi kwa ushirikiano na inapotokea kuna jambo linahitaji kushauriana tunashauriana kwa bamoja na kuheshimu mawazo ya kila mmoja wetu ili kufikia suluhisho," amesema Kunenge.


Pia Mhe, Kunenge amewataka wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Pwani kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kukuza uchumi.


''Natoa wito kwa wakuu wa wilaya wote nendeni mkaongeze nguvu katika kusimamia ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yenu ili mkoa wetu ufikie lengo tulilojiwekea". amesema Kunenge


Hafa ya kuapishwa kwa mkuu huyo wa wilaya iliyofanyika Kibaha, imehudhuriwa na watendaji mbalimbali wakiwamo wakuu wa wilaya za mkoa huo, baadhi ya viongozi wa CCM na viongozi wa dini.

Comments