MZEE WA MIAKA 92 ATUMIA FEDHA ZAKE KUJENGA KITUO CHA POLISI NA OFISI ZA KIJIJI KWA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 160.
FEDHA ALIZO ZIPATA KUTOKANA NA BIASHARA YA KILIMO PAMOJA NA MICHANGO YA MARAFIKI NA NDUGU.
Muktasari: Mzee huyo ambaye kwasasa ni mlemavu wa miguu kutokana na maradhi, amefanikiwa kujenga majengo hayo yenye thamani ya zaidi ya Sh160 milioni na kuyakabidhi kwa serikali..
Na Lucas Myovela -Arusha.
Katika hali isiyotarajiwa na wengi, mzee mwenye miaka 92, Aminieli Kuleiye Nko ameamua kutumia fedha zake za mfukoni kujenga majengo matatu, likiwamo la kituo cha polisi, jengo la ofisi ya serikali ya kijiji na la ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mzee huyo, ambaye kwa sasa ni mlemavu wa miguu kutokana na maradhi amesema ujenzi huo umegharimu jumla ya Sh160 milioni na leo amekabidhi majengo hayo kwa serikali tayari kwa kuanza kutumika.
Mzee huyo ambaye pia ni wa kimila wa Kabila la Wameru maarufu kwa jina la Kurii', akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda amesema alifikia uamuzi huo baada ya kubaini katika eneo hilo kuna uhitaji mkubwa wa kituo cha polisi na ofisi ya kijiji kwa sababu wananchi hutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za polisi na huduma za kiserikali zinafanyikia nyumbani kwa viongozi.
“Mimi napenda amani utulivu na usalama, lakini kadiri siku zinavyokwenda, usalama unazidi kupungua Nikaona kituo cha polisi kikiwepo hapa kitasaidia wanaovunja sheria kuchukuliwa hatua kwa haraka zaidi, nikaamua kujenga kituo hiki na ofisi hii," amesema mzee huyo.
Amesema ujenzi wa majengo hayo umegharimu zadi ya Sh160 milioni, huku kituo cha polisi kimejengwa kwa Sh60 milioni, ofisi ya kijiji Sh50 milioni na jengo la ofisi ya CCM limegharimu Sh50 milioni.
"Fedha hizi niliziwekeza kutokana na shughuli zangu za kilimo na biashara ya vibuyu, lakini pia michango ya ndugu, jamaa na marafiki walioona dhamira yangu ya kusogeza huduma kwa jamii," amesema Kuleiye Nko.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa ofisi ya CCM, Kuleiye Nko amesema;
"Wakati nakamilisha majengo hayo mawili, nikaona kuna uhitaji pia wa ofisi ya chama changu cha CCM, nikaamua kuijenga pia ili niache pia alama yangu ya kukipenda chama changu tangu nikiwa mdogo". Amesema.
Akipokea majengo hayo kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Kaganda, alimpongeza mzee Kuleiye Nko kwa kujitolea fedha zake kusudi atekeleze ujenzi huo akilenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa Kata ya Seela-Sing'isi.
"Huyu mzee aliona hapa kijijini kuna uhitaji wa kituo cha polisi na ofisi ya kijiji, akaja ofisini kwetu kuomba eneo la kujenga miundombinu hiyo, akaoneshwa na kweli amejenga na leo anatukabidhi majengo". Amesema
Ni jambo kubwa na la kizalendo na tunakushukuru sana kwa kutoa fedha zako zaidi ya Sh160 milioni kuisaidia serikali," amesema Kaganda.
Amesema hiki kilichofanya na mzee Kuleiye Nko kinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wengine badala ya kukaa vijiweni na kukosoa kila jambo linalofanywa na serikali.
Amesema kama mtu anaona anauwezo na anaweza kuisaidia Serikali kutekeleza jambo fulani, anaweza kufanya hivyo na afanye kama alivyofanya mzee huyo.
"Mzee huyu akawe mfano kwenu wa kuondoa ubinafsi mioyoni mwenu, kila mtu kwa nafasi yake akaone uhitaji wa mwenzake na kusaidia wengine. Mkifanya hivyo, mtaisaidia hata Serikali yenu pia,' amesema Kaganda.
Diwani wa Seela-Sing'isi, Elisa Nassari amesema majengo hayo yatapunguza usumbufu kwa wananchi wake kuwafuata viongozi nyumbani wanapotaka huduma za kiserikali ikiwemo usuluhishi au kugongewa mihuri kwenye nyaraka mbalimbali.
"Pia majengo haya yatapunguza matukio ya kihalifu kutokana na mkono wa sheria kusogea karibu, kwani itakuwa rahisi kwa wananchi kutoa taarifa na kushughulikiwa haraka tofauti na awali kituo kilipokuwa mbali hata gharama za kukifuata zilikuwa kubwa, sasa wataepuka gharama hizo," amesema Nassary.
Comments
Post a Comment