DKT. MAHERA AKEMEA VIKALI JAMII KUWANYANYASA WATU WENYE MAHITAJI MAALUMU.

 SERIKALI KUUNDA MABARAZA YA ULINZI NA USALAMA KUANZIA NGAZI YA KATA HADI MKOA.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Willson Charles Mahera, ameitaka jamii kupiga vita unyanyasaji na unyanyapaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kujenge jamii yenye usawa.

Dkt. Mahera ameyasema hayo jijini Arusha akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa kufunga Maadhimisho ya Miaka ya 30 ya Elimu Jumuishi hapa nchini ambapo amesema kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wenye mahitaji maalum kielimu.


Dkt. Mahera amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa lengo naomba 4 la malengo ya milenia ya mwaka 2030 linalosisitiza usawa pamoja na kutekeleza Azimio la Musoma la mwaka 1974, ambalo lililochagiza kila Mtanzania kupata fursa ya elimu.

Aidha Dkt. Mahera ameeleza kuwa Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi Serikali imefanikiwa kuyafikia makundi yote ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wanafunzi wenye ulemevu, magonjwa ya kudumu pamoja na wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini.


"Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa miongozo inayoelekeza wadau wa elimu kutoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji Maalum hususan wenye kiwango kikubwa cha ulemavu" Alibainisha Dkt. Mahera.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anaye shughulikia elimu Atupele Mwambene amewaasa Maafisa Elimu Maalum wa Wilaya kuhakikisha wanaelewa vyema mikakati na miongozo ya utekelezaji wa elimu Jumuishi ili kuwa na ufanisi mzuri wa majukumu yao.


Mwambene amesema Serikali itaitekeleza kwa vitendo na kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanajengewa maadili mazuri kwa kuimarisha vituo vya malezi, ushauri na unasihi ili viweze kutoa huduma nzuri.


"Tutaendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la ubainishaji wa Watoto wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha wanaandikishwa shule na kupatiwa afua stahiki kulingana na mahitaji waliyonayo". Alisema Mwambene.













Comments