WANANCHI ARUSHA WAJITOKEZA KWA WINGI KUJIANDIKISA KATIKA DAFTARI LA MPIGA KURA.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Arusha Mjini, John Kayombo ameongoza mamia ya wakazi wa jimbo hilo kujiandikisha katika daftari la Mpiga kura katika kituo cha shule ya sekondari Olorien na kuwahimiza wananchi ambao bado kutumia fursa hiyo ili kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27 Mwaka huu.

Akiwa katika kituo hicho Kayombo ameeleza namna zoezi hilo linavyoendelea vizuri na kwamba katika vituo 40 alivyotembelea hakuna changamoto wala malalamiko yoyote yaliyojitokeza.


Kayombo ambaye pia ni Mkurugenzi wa jiji la Arusha, amewataka mawakala wa vyama vya siasa ambao hawakupata fursa ya kula kiapo kwa wakati ,ametenga chumba maalumu cha kuwaapisha ofisini kwake na kuwataka kwenda kula viapo ili kushiriki zoezi hilo kwa uaminifu.


Mwandikishaji katika kituo cha Moivoi kata ya Olorien, Rose Mkundi alisema katika kituo chake zoezi linaenda vizuri na mwitikio ni mkubwa.


"Tangu tumefungua kituo mwitikio ni mzuri na watu wanaendelea kujiandikisha kwa wingi"


Mmoja ya wananchi Vedeus Masawe mkazi wa Moivoi alipongeza utaratibu iliotumika katika kujiandikisha kwani wananchi wanachukua muda mfupi wa dakika tatu kujiandikisha na kwenda kwenye majukumu yao.


"Utaratibu uliotumika umesaidia sana watu kuto kukaa kwenye vituo kwa muda mrefu na kutumia muda mfupi ,mimi nimetumia dakika tatu na kuondoka"


Alisema suala la kujiandikisha ni jambo la msingi sana litakalo mwezesha mwananchi kutumia haki yake ya msingi kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowahitaji.


Zoezi hilo la kujiandikisha limeanza leo Oktoba 11 hadi oktoba 20 Mwaka huu majira ya saa mbili hadi saa 10 jioni ambapo kitaifa limeongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Comments