BODI YA MIKOPO YAWEZESHA WANAFUNZI ZAIDI YA 400,000 KWA MWAKA WA MASOMO 2024-2025.

🔻MSTAHIKI MEYA AZINDUA MAONESHO YA BODI YA MIKOPO (HESLB) KANDA YA KASKAZINI.

🔻AIPONGEZA BODI KWA UTOAJI HUDUMA ZA MIKOPO KWA WANAFUNZI KWA NJIA YA KIDIGITI.

Na Lucas Myovela - Arusha.

Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe.Maxmillian Matle Iranqhe amezindua maonesho ya Bodi ya Mikopo(HESLB) kanda ya Kaskazini ambayo makao yake makuu ni Jijini Arusha kuelekea kilele cha miaka 20 ya bodi hiyo toka kuanzishwa kwake hapa nchini.

Akizindua Maonyesho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Mhe. Paul Makonda, Mhe. Iranqe ameipongeza bodi hiyo ya mikopo kwa kutimiza miaka 20 toka ianzishwe kwake na kwa kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi wa vyuo.


Iranqhe amesema kuwa bodi hiyo ya mikopo inatimiza miaka 20 huku ikiwa imeisaidia jamii ya Watanzania wengi wenye kipato cha chini kwa kupata elimu ya juu kitu ambacho kimeongeza idadi ya wasomi wengi nchini na wataalamu wa fani mbalimbali.


"Bodi hii tangu kuanzishwa kwake hadi kufikia mwaka wa masomo 2024/2025, bodi hii imewezesha takribani Wanufaika zaidi ya laki nane (400,000) kupata elimu katika ngazi ya vyuo vikuu na vyuo vya kati kama serikali yetu ilivyo agiza na wanafunzi wote wenye sifa za kupata mikopo hii wanajua namna gani inavyo wasaidia katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kiada na kitaaluma vyuoni". Amesema Iranqhe.


Aidha Iranqhe ameeleza kuwa bodi hiyo imeweza kuboresha mifumo yake ya utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa wanafunzi kutoka kutumia nakala ngumu (karatasi) kuomba mkopo hadi sasa kutumia njia ya mfumo wa Kidigiti (online system) kuomba mkopo, kupanga mikopo na kurejesha mikopo hiyo katika bodi.


"Niweze kuwapongeza kwa kupiga hatua kubwa na kuondoa changamoto mbalimbali za uombaji mikopo kwa kutoka katika maombi ya barua za mkono hadi kutumia mifumo ya kimtandao ili kuharakisha upatikanaji wa mikopo kwa waombaji hata kwa wale wanufaika pindi wanapo rejesha mikopo yao kutumia njia mfumo wa kimtandao ambayo ni salama, rahisi na haraka". Amesema Iranqhe.


Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya mikopo kanda ya Kaskazini Lucy Kirigha, Ameeleza kuwa uwepo wa maonyesho hayo ni kuwajengea uwezo na uelewa watanzania wanaotaka kujiendeleza katika elimu ya juu ili kuweza kujua ni namna gani wataweza kunufaika na mikopo hiyo katika kujiendeleza kitaaluma.


"Uwepo wa maonyesho haya ni chachu kubwa kwa watanzania kuijua bodi ya mikopo inafanyaje kazi zake na kutoa mwangaza kwa wanafunzi ambao hawajui namna ya kuomba mikopo, Pia ni fursa kwa wale ambao hawajui waanze vipi kuomba mikopo ya elimu ya juu, kwetu sisi wote tunawapokea na tuna wahudumia vyema ili waweze kunufaika". Amesema Kirigha.


Aidha Kirigha ametoa wito kwa Watanzania wenye sifa za kupata mikopo kutosita kuomba mkopo pindi dirisha la kuomba litakapofunguliwa ili waweze kujiendeleza kitaaluma na taifa liweze kunufaika kwa kupata wataalamu wenye ubora.


Maonesho hayo ya bodi ya mikopo Kanda ya Kaskazini yameshirikisha taasisi za elimu ya juu pamoja na taasisi za kifedha kwa lengo la kuwaweka wadau wote wa elimu pamoja na kuwa na dira moja ya maendeleo ya elimu ya juu kwa kutatua changamoto za kifedha na kitaaluma nchini.


Taasisi za kifedha zilizo shiriki maonyesho hayo ni NMB Benki, CRDB Benki. Huku taasisi za elimu zilizo weza kushiriki ni Tengeru Institute of Community Development (TICD), Arusha Technical College (ATC), Chuo kikuu cha SAUT, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Chuo kikuu cha Arusha, Chuo kikuu cha Tumaini.


Pia Taasisi zingine zilizo weza kushirini ni Chuo cha Madini,Chuo cha Uhifadhi na Utalii MWECAU, TANAPA, UTT-AMIS na NHIF.







Comments