🔻AKEMEA UNYANYASAJI NA UKATILI UNAO TOKANA NA BAADHI YA TAMADUNI HAPA NCHINI.Na Lucas Myovela - Arusha.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Dkt. Doroth Gwajima ameupongeza Mkoa wa Arusha kwa maandalizi mazuri kuelekea wiki ya wanawake duniani, akihimiza jitihada zaidi kwenye utekelezaji wa mikakati ya kuwainua wanawake katika nyanja mbalimbali pamoja na kuondoa unyanyasaji na ukatili wa aina mbalimbali kwa wanawake na wasichana.
Wakati akizungumza na wajumbe wa kamati mbalimbali za maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya mwanamke duniani Machi 08, 2025, Waziri Dkt. Doroth Gwajima amesisitiza pia umuhimu wa Mkoa wa Arusha na mikoa mingine kote nchini, kuendelea kutoa elimu ya afya, Mikopo kwa wanawake sambamba na kuwafahamisha wananchi kuhusu fursa za uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Akikemea udhalilishaji na ukatili wa kijinsia unaotokana na baadhi ya tamaduni katika Mikoa ya Arusha na Manyara inayopelekea ukeketaji kwa wasichana, Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa kubuniwa mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili huo ili kubadilisha sura na takwimu za unyanyasaji katika Mikoa hiyo pamoja na kutokomeza fikra na tamaduni za kale zisizokuwa na faida kwa zama hizi.
Kikao hicho pia kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, kilihudhuriwa na washauri wa Rais Mhe. Angellah Kairuki pamoja na Mhe. Sophia Mjema, Katibu tawala Mkoa wa Arusha Musa Missaile, wadau mbalimbali kutoka Taasisi za kifedha na wa masuala ya wanawake pamoja na Viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi CCM na serikali.
SERIKALI YAKOSHWA MAANDALIZI KABAMBE SIKU YA WANAWAKE ARUSHA.Aidha katika hatua nyingine Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi maalum Dkt. Doroth Gwajima amefika Mkoani Arusha na kukagua maandalizi ya Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ambayo kitaifa yatafanyika Mkoani Arusha, akiridhishwa na maandalizi mazuri na kutangaza kuwa Kiwango cha maandalizi yanayofanywa Mkoani Arusha kitakuwa kiwango cha kutolewa mfano kwenye maadhimisho yajayo.
Waziri Gwajima aliyeambatana na washauri wa Rais Mhe. Sophia Mjema na Mhe. Angellah Kairuki, wakati akizungumza na Kamati za maandalizi ya maadhimisho hayo Jijini Arusha, ameagiza kuandaliwa kwa Kamati ndogo itakayoangazia maandalizi ya maadhimisho hayo ngazi ya Mkoa na kuahidi kutangaza Mikoa iliyofanya vizuri mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, anayetarajiwa kuwa Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo kwa mwaka huu.
Maadhimisho ya kitaifa ya siku ya wanawake duniani yatafanyika Machi 08, 2025,Jijini Arusha kwenye viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid Karume, Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo kabla ya kilele chake kwa wiki nzima kutafanyika shughuli mbalimbali Mkoani humo ikiwa ni pamoja na elimu mbalimbali, msaada wa kisheria pamoja na mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo ya magari itakayohusisha wanawake.
Comments
Post a Comment