WANA ARUSHA WAASWA KUCHANGAMKIA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA.
Na Lucas Myovela - Arusha.
Akizungumza leo Machi 1, 2025, jijini Arusha wakati alipotembelea mabanda mbalimbali yanayotoa huduma za msaada wa kisheria chini ya kampeni hiyo, Sagini alisema ameridhishwa na maandalizi ya mkoa huo pamoja na utaratibu mzuri uliowekwa kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi wengi.
"Ninafarijika kuona maandalizi ya mkoa wa Arusha yanatia moyo. Nawapongeza viongozi wa mkoa, mkurugenzi na timu nzima kwa jinsi walivyojipangakuhakikisha huduma hizi muhimu za msaada wa kisheria zinatolewa kwa ufanisi," amesema Sagini.
Aidha, amewataka wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kupata msaada wa kisheria kwani kuna wataalamu mbalimbali waliopo kwa ajili ya kuwahudumia, wakiwemo wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Tanganyika Law Society (TLS), Jumuiya ya Mawakili wa Serikali, taasisi mbalimbali za kisheria pamoja na mawakili binafsi.
Lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu juu ya masuala ya kisheria pamoja na kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi.
"Nimeona watu wengi wanahitaji huduma za kisheria, na jambo la kufurahisha ni kuwa sekta zote muhimu za kisheria zipo hapa kushirikiana ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora," ameongeza Sagini.
Kwa wananchi wa Arusha wanaoishi maeneo ya vijijini na watakaoshindwa kufika kupata huduma hizo kwa siku zote nane(8), Sagini amesema Wizara ya Katiba na Sheria itafanya tathmini na kupanga utaratibu wa kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia katika wilaya zote za mkoa wa Arusha.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu, kinatarajiwa kufanyika kitaifa tarehe 8 Machi 2025, mkoani Arusha, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Comments
Post a Comment