MIAKA 61 YA MUUNGANO DKT. BITEKO AHIMIZA VIONGOZI KUACHA ALAMA.

🔻DKT. BITEKO AAGIZA KUWEKWA MFUMO WA UMEME WA DHARURA KATIKA KITUO CHA KUSUKUMA MAJI NAMBA 5 CHEKERENI JIJINI ARUSHA.

Na Lucas Myovela - Arusha.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kuishi kwa upendo na kushirikiana kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.


Amesema katika kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano ambapo amewahimiza Watanzania kukumbuka kuwa kuwa Mwl. Julius Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume waliunganisha Tanganyika na Zanzibar katika misingi ya umoja, amani, ushirikiano na kuheshimiana hivyo, muhimu kuendeleza misingi hiyo ili kuenzi Muungano.


Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 26, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Soko la Kilombero, Wilaya ya Arusha Mjini, Mkoa wa Arusha. 


"Arusha mfanye kazi kwa kushirikiana, muijenge Arusha yenu mkumbuke kwenye nafasi zetu za uongozi mjue kesho hamtakuwepo mtaondoka, kila mahala ulipo acha alama njema itakayo kumbukwa na wengine". Amesema Dkt Biteko.


"Sisi tuliopo leo tutakumbukwa kwa lipi, iwe changamoto tunapokumbuka miaka 61 ya Muungano tujue ni alama gani tutaacha kwa watoto wetu," Ameongeza Dkt. Biteko.

Amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025 Watanzania waishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana na kuwa wamoja kwa kuchagua viongozi wanaoweza kuwasilisha ajenda zao kwa wananchi.


"Hicho ndicho kiwe kipimo na viongozi tusitumie tofauti zetu kutafuta kura, usiende kanisani au msikitini kwako kutumia uhalali watofauti zetu kutafuta kura asitokee yeyote kufanya hivyo tuuenzi Muungano na Rais Samia ameapa kuulinda Muungano huu kwa wivu mkubwa," amesema Dkt. Biteko.


Dkt. Biteko amebainisha Watanzania wasiruhusu Taifa kugawanyika kwa sababu yoyote ile wakumbuke kuwa

kama hakuna amani hakuna biashara wala maendeleo yanayoweza kufanyika.


NAIBU WAZIRI MKUU AKAGUA KITUO CHA KUSUKUMA MAJI SAFI ARUSHA.

Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametembelea Kituo cha Kusukuma Maji namba tano cha Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kilichopo Chekereni, Aprili 26, 2025 Arusha.


Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko ameagiza Kuwekwa mfumo wa umeme wa dharura (backup) katika kituo hicho,Kuimarishwa kwa juhudi za kudhibiti upotevu mkubwa wa maji na Kuboresha huduma za maji kwa wananchi.


Aidha, Dkt. Biteko amekagua maendeleo ya miundombinu ya mradi huo na kupanda mti wa kumbukumbu katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi Mkoa wa Arusha (AUWSA) Mhandisi Justine Rujomba akitoa maelezo ya namna kituo hicho kinavyo pokea maji na kuyasambaza katika vituo vingine mbele ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Dotto Mashaka Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akikabidhi mtungi wa gesi kwa Baba lishe Raphael Msele katika viwanja vya soko la Kilombero katika Manispaa ya Arusha Aprili 26, 2025 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 61 ya Muunaano wa Tanzania.

Comments