🔻Ailekeza TANESCO kufunga Kituo cha Kupoza Umeme Longido.
🔻Amuagiza Makonda kusimamia ufungaji vifaa vya maabara Sekondari ya Longido Samia.
Na Lucas Myovela - Arusha.
“ Nimefurahishwa sana na urahisi wa biashara na kila eneo limekuwa na ukuaji wa watu na bidhaa kwenye kusafirisha nje ya nchi ili kuleta fedha ya kigeni zitakazowezesha kufanya shughuli zingine nawapongeza sana, nawashukuru kwa kuwa na malengo makubwa ya kukusanya shilingi bilioni 124 na hadi kufikia leo mmekusanya shilingi bilioni 101 huku mkiwa na miezi kadhaa ya kuendelea kukusanya mapato” amesema Dkt. Biteko.
Amewataka watendaji hao kuendelea kuwa na utaratibu mzuri wa kurahisisha biashara kwa kuondosha mizigo inayosafirishwa kwa kutumia muda wa dakika 30 hadi 40 badala ya saa 2 kama ilivyokuwa hapo awali.
Ameendelea kusema kuwa Kituo hicho cha Namanga kilichofunguliwa mwaka 2018 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dkt. John Pombe Magufuli na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta kwa lengo la kurahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili. Hivyo, watendaji hao waendelee kuwa mabalozi wazuri kwa kutangaza taswira njema ya Tanzania wakati wakitekeleza majukumu yao.

Pia, Dkt. Biteko amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda kuhakikisha Shule hiyo inapata vifaa vya maabara ili wanafunzi waweze kujifunza kwa vitendo na si nadharia pekee.
Katika maelekezo yake kwa mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda Mhe. Biteko amemtaka kuangalia namna ya kuweka uzio na kupata gari kwa ajili ya shule hiyo, huku akiwataka wanafunzi kujifunza kwa bidii ili watimize ndoto zao na kuwa Shule hiyo ni kielelezo cha Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo, Esther Kobelo, amesema shule hiyo ni mojawapo ya shule 26 mpya zilizoanzishwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni juhudi za serikali kuendeleza elimu nchini, ambapo shule hiyo ilifunguliwa Januari 7, 2024, ikiwa na wanafunzi 310 wa kidato cha kwanza na cha tano, wote wakisomea masomo ya sayansi. Shule ina walimu 16, ambapo walimu wa kike ni wanne tu, pamoja na mtaalamu mmoja wa maabara.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mundarara, Dkt. Biteko amesema madini ni kichocheo kikubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kuwa Kijiji cha Mundarara kimekuwa na uzalishaji wa madini ya rubi na kuwa anafurahishwa kwa kuona sasa Watanzania wanaweza kufanya kazi za uchimbaji wa madini.
Vilevile, Dkt. Biteko ameelekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujenga njia nne za kupeleka umeme Loliondo, Namanga, Mundarara na Kamwanga na baadae kujenga kituo cha kupokea, kupoza na kusafirisha umeme ili kusaidia wananchi kupata umeme na kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Pamoja na hayo, amesema kuwa Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuwaletea Watanzania maendeleo na kuwaasa wamuunge mkono. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu kwa kuchagua viongozi watakao waletea maendeleo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amebainisha kuwa katika kusheherekea miaka 61 ya Muungano ni vyema kila Mtanzania ajiulize kwa nafasi yake, amefanya nini yeye binafsi, lakini pia amefanya kitu gani hasa cha kukumbukwa kwa watu wake wa karibu, kwa jamii inayomzunguka na pia kwa Taifa.
Ameendelea kusema Wilaya hiyo imenufaika na miradi ya maendeleo ambapo usanifu wa barabara ya kutoka Siha hadi Longido unaendelea.
Amesisitiza “ Wilaya hii tumepewa fedha ya kujenga shule za sekondari sita katika kata zetu na tumebakiza kata tatu ambazo hazina shule za sekondari, kazi ya kujenga shule katika kata hizo inaendelea. Mafanikio haya yasingeweza bila kuwa na ushirikiano na mshikamano kati aya Chama Cha Mapinduzi, Serikali na viongozi wa kimila.”
“ Tayari fedha zaidi ya shilingi milioni 250 imetolewa na baada ya wiki moja itaonekana kwenye mfumo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya. Kuhusu barabara, katika bajeti hii imetengwa fedha shilingi milioni 270, fedha hizi ni kwa ajili ya barabara ya Resingita yenye urefu wa km 13 na barabara ya Longido kwenda Meloe imetengewa shilingi milioni 105,”amesema Mhe. Makonda.
Comments
Post a Comment