SERIKALI YA CANADA NA TANZANIA KUSHIRIKIANA KUHAKIKISHA VIJANA WALIYO KATIZA MASOMO KUTIMIZA NDOTO ZAO.

🔻WAPATA MAFUNZO KATIKA VYUO MBALI MBALI NCHINI  ILIKUWEZA KUJIKWAMUA KIUCHUMI. 

Na Lucas Myovela - Arusha.Mpango wa Uwezeshaji Ujuzi (ESP) umewezesha jumla ya wanawake na wasichana 720 kujifunza programu za muda mfupi za kijinsia, upishi na Tehama ikiwemo serikali kuandaa mitaala 20 inayolenga jamii kujikwamua kiuchumi.Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kupitia hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Charles Mahera wakati akifungua Jukwaa la Ushirikiaono la ESP mwaka 2025 Jijini Arusha.


Prof. Mkenda ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kanada zitaendelea kushirikiana katika kuhakikisha vijana waliokatisha masomo wanatimiza ndoto zao kupitia mafunzo mbalimbali ya ujuzi ili kujikwamua kiuchumi kupitia vyuo 12 kati ya 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs).

"Vyuo hivi vimekuwa wanufaika kupitia mradi wa ESP kwa kutoa mafunzo na kuboresha ushiriki wa wanawake na wasichana kwenye shughuli za kiuchumi nchini kwa kuwapatia ujuzi mbalimbali kama upishi, Tehama, usindikaji wa vyakula na vingine vingi". Amesema Mkenda.

 

"Mpango wa ESP umekuwa kichocheo kikuu katika kutekeleza dhamira hii, Tunasherehekea ushirikiano unaoleta pamoja taasisi 16 za Kanada na taasisi 24 za Tanzania ikiwa ni pamoja na Vyuo 12 vya Maendeleo ya Wananchi katika mikoa yetu, na Mashirika 12 ya Kijamii yanayofanya kazi katika ngazi ya jamii, Mbinu hii jumuishi inaakisi uelewa wa kina kwamba uwezeshaji wa kweli lazima uwe shirikishi, unaozingatia muktadha wa ndani ya nchi," Ameongeza Profesa Mkenda .


"Kipekee ninawashukuru Serikali ya Kanada, The Global Affairs Canada, Vyuo na Taasisi za Kanada kwa ushirikiano wenu thabiti. Hamjaleta rasilimali tu bali pia mmeshirikisha utaalamu, mshikamano na maono. Pia natoa shukrani kwa timu nzima ya ESP, kazi yenu inabadilisha maisha ya vijana na wanawake nchini." Amesisista Prof. Mkenda.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Jumuiya ya Vyuo na Taasisi za Ufundi Kanada (CICan) nchini, Dkt. Alice Mumbi amesema kuwa Jukwaa hilo limewaleta pamoja washiriki zaidi ya 100 wa ndani na kimataifa. 


Dkt. Mumbi ameeleza kuwa kwasasa ni mwaka wa tano na ESP imepiga hatua kubwa katika kuandaa na kutekeleza kozi fupi kulingana na mahitaji zikiwemo kozi za Tehama,Ujaliamali na uundaji wa vifaa, ujuzi wa upishi na vituo vya kulelea watoto mchana (Day Care) pamoja na masuala ya usawa wa kijinsia.


"Ushirikiano wetu wa ndani na wa kimataifa ndio kiini cha programu hii, Jukwaa hili ni ushuhuda wa nguvu ya ushirikiano katika kuendeleza maendeleo endelevu ya ujuzi jumuishi ambayo yanawawezesha wanawake kiuchumi na kubadilisha jamii," amesema Dkt. Mumbi.


Naye Dkt. Paula Hayden ambaye ni Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa ESP-TVET ameeleza kuwa ESP ni mpango unaohimiza usawa na fursa, hivyo jukwaa hilo linaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya nchi mbalimbali, sekta, na jumuiya kuwajengea ujuzi kwa vitendo vijana na wanawake kwa ustawi wa maisha yao.


Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi Wizara ya Elimu Dkt. Fredrick Salukele, Ameeleza kuwa mpango huo unalenga kujenga uwezo katika usawa wa kijinsia, haki za binadamu, mbinu za ufundishaji na mafunzo ya watu wazima, uendelevu wa mazingira, uongozi, mwongozo na ushauri wa kazi, afya na usalama wa kazi, masoko, kujiajiri na Tehama (ICT).


Akizungumza kwa niaba ya wakurugenzi wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Bi, Ester Chaula amesema kwamba mradi huo umeboresha matumizi ya Tehama ambao umeleta manufaa kwa wakufunzi na wanafunzi ikiwemo mafunzo ya usawa wa kijinsia, kozi za muda mfupi za upishi, ushonaji na usindikaji wa vyakula mbalimbali.


Naye Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Kanada nchini, Carol Mundle alisema nchi hiyo itaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa wasichana ili waweze kujikwamua kiuchumi pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa shule za awali ili kuwezesha ukuaji wa elimu na wazazi kujikwamua kiuchumi kupitia programu hiyo


Kwa upande wake, Meneja wa Operesheni, Caribbean na Anglophone Africa-CICan Ottawa, Alina Scutaru alibainisha kuwa jukwaa hilo ni fursa muhimu kwao kutafakari, kuungana na kupanga mipango yao kwa kuwa maendeleo waliyofikia yasingewezekana bila kujitolea, ubunifu na ushirikiano huo.













Comments