UWEKEZAKI WA CRDB BANK WAFIKA TRILIONI 17.6.

KAMA NI MWANAHISA CRDB HII UMETOBOA KWA GAWIO NONO.

Na Lucas Myovela - ARUSHA.

ARUSHA; Benki ya CRDB, Imefikia uwekezaji wa thamani ya Shilingi Trilioni 17.6 na kupata faida ya shilingi Bilioni 173 kwa robo ya mwaka wa mwezi machi 2025, huku Wanahisa wa Benki ya CRDB wanatarajiwa kunufaika na gawio la Shilingi 65 kwa kila hisa kwa mwaka 2025 baada ya benki hiyo kupata faida ya shilingi Bilioni 551 baada ya kodi kwa mwaka 2025.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Arusha leo Mei 14, 2025 kuelekea mkutano mkuu wa 30 wa benki ya CRDB wenye kauli mbinu 'miaka 30 ya ukuaji pamoja ' unaotarajiwa kufunguliwa na makamu wa Rais Dkt Philipo Mpango Mei 17, 2025 katika kituo cha AICC jijini Arusha.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB, Dkt. Ally Laay, ameeleza kuwa kutokana na faida hiyo bodi ya wakurugenzi imependekeza gawio la shilingi 65 kwa kila hisa ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 30, kulinganisha na gawio la mwaka jana 2024 ambalo lilikuwa ni shilingi 50 kwa hisa.

"Gawio hili litaidhinishwa na wanahisa wenyewe wa benki ya CRDB na Benki itatoa gawio la jumla ya shilingi bilioni 169.8 kwa wanahisa wote kwa mwaka huu 2025 na hii itavunja rekodi zote zilizopita miaka ya nyuma hii inatokana na kukua kwa benki kila mwaka". Amesema Dkt. Laay.


"Kutokana na faida hiyo, Mkutano Mkuu wa 30 wa Wanahisa wa benki uliopangwa kufanyika Jumamosi mei 17, 2025 katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha AICC jijini Arusha pamoja na mambo mengine, unatarajiwa kupitisha pendekeo hilo la ongezeko la gawio kwa hisa linalotokana na benki kuendelea kupata matokeo mazuri sokoni". Ameongeza Dkt. Laay.

Aidha Dkt. Laay ameleeza kuwa mbali na kuwepo ajenda mbalimbali zitakazo jadiliwa katika mkutano huo pia kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe huru wa bodi, kuteua wakaguzi wa hesabu, kujadili na kupokea Taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi, Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa na gawio kwa mwaka 2025 ambapo mkutano huo pia utafanyika kwa njia mseto ili kutoa fursa kwa wanahisa wengi zaidi kushiriki kwa njia ya kidigitali.


"Kupitia njia ya mtandaoni wanahisa wataweza kujiunga kuanzia saa 2:00 asubuhi kupitia tovuti ya benki hiyo au mfumo wa benki hiyo waliopakua katika simu au kompyuta zao tayari tumeweka mwongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yetu, mitandao yetu ya kijamii, pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa wanahisa". Amesema Dkt. Laay.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, meeleza kuwa thamani ya uwekezaji wa benki ya crdb imekuwa na kufikia shilingi za kitanzani Trilioni 17.6, na kuweza kupata faida ya shilingi Bilioni 173 hadi robo ya kwanza ya mwaka kutoka mwezi Januari hadi mwezi machi 25, 2025.


Nsekela ameeleza mkakati wa kuendelea kufungua matawi ya benki hiyo nje ya nchi ambapo kwasasa wamefanikiwa kufungua tawi katika nchi ya Burundi ma tawi hilo linalofanya vizuri zaidi na kuifanya kuwa benki kinara katika nchi hiyo.

"Benki yetu imefanikiwa kuingia nchi ya DR Kongo na Tayari tumefungua matawi katika miji ya Kinsasa na Lubumbashi ambayo yanaendelea vizuri, mpango wetu mwingine ni kufungua tawi katika nchi ya Dubai na tayari tumeshapata kibali na mchakato wa kupata eneo la kufungua tawi la CRDB unaendelea na  mipango mikubwa ni kufungua matawi katika nchi mbalimbali za Afrika unaendelea". Amesema Nsekela.


"Thamani hisa ya benki yetu imeongezeka baada ya kuwepo kwa hamasa kubwa kwa ununuzi wa hisa kwa mtu mmoja mmoja hii ni kutokana na maboresho ya miundo mbinu, ubunifu mkubwa na kuongezeka kwa mapato na kubana matumizi kitu ambacho kimetugikisha katika mafanikio haya ambayo wanahisa wanaenda kunufaika nayo". Ameongeza Nsekela.


Aidha Nsekela amewataka wanahisa wote wa Benki ya CRDB kujitokeza kwa wingi kwa kuwa ushiriki wao utawezesha Bodi na Menejimenti kupata maoni yao ya namna bora ya kuboresha huduma za kibenki na kuweka mawazo ya pamoja na muelekeo wa benki hiyo kwa ukuaji kimapato na huduma bora kwa wateja.








Comments