KIHONGOSI ATAKA AMANANI NA MSHIKAMANO, AMUAGIZA MKURUGENZI KUTOA ELIMU YA MIKOPO.
Na Lucas Myovela -Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi amewahimiza wafanyakazi wa saloon na waajiri kulinda tunu ya Taifa pamoja na amani iliyopo nchini na kuwataka kufanya kazi kwa kanuni na sheria za nchi.
Rc Kihongosi ameyasema hayo mapema leo alipokuwa akiongea na wamiliki, wafanyakazi wa saloon katika Jiji hilo kwa lengo la kubaini changamoto zao na kutafutia utatuzi sahihi ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza pamoja na kusisitiza suala la usafi wa maeneo wanayofanyia kazi.
"Nchi yetu ya Tanzania ni tunu pekee inayostahili kulindwa kwa watu mbalimbali niwaombe vijana wezangu pamoja na mama zangu msikubali kurubuniwa na kuipoteza amani iliyopo kwani baadhi ya watu wakiona wameharibu amani iliyopo wanakimbilia nchi za nje na kuacha wenzao wakitaabika hapa nchini". Amesema Kihongosi.
Kihongosi ameeleza kuwa watu wa saluni ni kada nzuri yenye wateja wengi hivyo wanapoona kunahabari tofauti za wateja wao watoe taraifa serikalini ili hatua ziweze kuchukuliwa na kusisitiza kulinda amani kwa kutoa viashiria ambavyo havijakaa sawa.
"Niwaombe waajiri wa saloon kutoa mikataba ya ajira, Jiji la Arusha limepewa na serikali shilingi bilioni 5.5 kwaajili ya utoaji mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kwa vijana, wanawake na makundi maalum kwaajili ya kupata mikopo hiyo ili wajikwamue kiuchumi". Ameeleza Kihongisi.
Nae Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, ameeleza kuwa mikakati ya Jiji hilo ni kuendelea kutoa elimu ya mikopo hiyo ili vijana wanapoichukua ikawajenge kiuchumi.
"Mikopo hii mkiichukua kwa malengo itawasaidia na itasaidia kukuza kipato cha kila mmoja wetu, Niwahakikishie tumejipanga vyema kuhakikisha tunawahudumia na kuwapa elimu ya usimamizi wa fedha ili Arusha yetu iwe imara kiuchimi".Ameeleza Kayombo.
Awali wananchi hao wakitoa changamoto zao wameeleza kuwa kwasasa kumetokea wafanya biashara kufanya kazi ya ususi nje ya milango yao kitu ambacho kinawakosesha wateja na kuiomba serikali kukomesha jambo hilo ili kila mmoja apate kidogo na kuendeleza amani.
Comments
Post a Comment