JUMLA YA BILIONI 33 KUTUMIKA HADI KUKAMILIKA MRADI HUO.
Na Lucas Myovela - Arusha.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, leo Julai 22, 2025 ametembelea eneo la ujenzi wa jengo la kisasa la ghorofa nane la Kituo cha Jiomolojia Tanzania (TGC), linaloendela kujengwa jijini Arusha, kwa lengo la kukagua maendeleo ya mradi huo muhimu kwa Sekta ya Madini nchini.
Katika ziara hiyo, Waziri Mavunde amepata fursa ya kujionea hatua mbalimbali za ujenzi na kupokea taarifa ya maendeleo kutoka kwa mkandarasi Julian Mosha wa Skywards Lumocons Joint Venture pamoja na wasimamizi wa mradi Jumanne Nshimba kutoka TGC ambapo baada ya kukamilika kwake unatarajiwa kuwa kitovu cha huduma za utambuzi wa madini, tafiti na mafunzo kuhusu vito vya thamani na madini mengine nchini, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini.
Amesema Jengo hilo linatarajiwa kuwa na madarasa ya wanafunzi, karakana, mabweni ya wanafunzi, maabara ya madini pamoja na ofisi mbalimbali kwa ajili ya uongozi wa chuo hicho ambapo zaidi ya bilioni 33 zinategemewa kukamilisha mradi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ukaguzi huo, Mhe. Mavunde ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa lakini amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
“Mradi huu ni wa kimkakati kwa mustakabali wa Sekta ya Madini nchini ambao utawaleta pamoja wafanyabiashara wa madini (One Stop Centre) Tunahitaji kuona ujenzi ukikamilika haraka ili Kituo hiki kianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa. Natoa wito kwa mkandarasi kuongeza nguvu kazi, vifaa na ufanisi ili kuendana na muda wa mkataba,” amesema Waziri Mavunde.
Mradi huu unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na taasisi ya TGC, ambapo jengo hilo litakapokamilika litaongeza uwezo wa kitaifa wa kuchambua madini, kutoa mafunzo ya kitaalamu, na kukuza ajira kwa vijana wa Kitanzania waliobobea katika masuala ya Jiolojia na Jiomolojia.
Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha miundombinu ya kisayansi na kiteknolojia kwa ajili ya matumizi bora ya rasilimali za madini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uongezaji thamani madini katika Ukanda wa Afrika.
Sambamba na hayo, Waziri Mavunde amekutana na kufanya kikao na Chama cha Wafabyabiashara Wadogo wa Madini ya Vito Arusha na Wachimba wa Madini kwa lengo la kusikiliza change motor za na kuzitolea ufunmbuzi.
Awali, Waziri Mavunde alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi kwa lengo la kupata taarifa za shughuli za madini zinazoendelea mkoani humo ambapo Kihongosi amempongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya Sekta ya Madini katika Mkoa wa Arusha hususan mradi wa ujenzi wa Jengo la kisasa la ghorofa nane la TGC na kumpongeza kwa kuvuka lengo la makusonyo ya maduhuli ya Serikali.
Comments
Post a Comment