VIJANA 423 WARASIMISHWA MYORORO WA UCHIMBQJI NA UUZAJI WA MADINI YA TANZANITE.

 🔻RAIS. DKT. SAMIA KUIMARISHA UCHUMI WA VIJANA KUPITIA SEKTA YA MADINI VKUNDI 21 VYA VIJANA WAPEWA LESENI MANYARA.

🔻Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa madini kupitia programu jumuishi ya Mining for Better Tomorrow (MBT), inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake kunufaika moja kwa moja na rasilimali za taifa.

Na Lucas Myovela - Manyara.

Zaidi ya vikundi 21 vya wachimbaji wadogo wa madini vyenye wanachama zaidi ya 423 vimepewa leseni za uchimbaji katika kijji cha Lemshuku, wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kupitia programu jumuishi ya Mining for Better Tomorrow (MBT).


Leseni hizo zilizogawanywa katika makundi mawili zimetolewa kwa vikundi saba vya uchimbaji wa Tanzanite vyenye wanachama zaidi ya 125 huku leseni nyingine zikikabidhiwa kwa vikundi 14 vyenye wanachama zaidi ya 295 ambavyo vinajishughulisha na biashara ya madini hayo kwa upande wa kuuza na kununua.


Utolewaji wa leseni hizo ni hatua ya kuwarasimisha wanachama wa vikundi hivyo kufanya biashara katika mnyororo wa thamani wa madini hayo kupitia vikundi vyao hali inayotarajiwa kuongeza ajira rasmi na kukuza uchumi wa wachimbaji na wauzaji hao sambamba kuongeza pato la taifa.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akikagua ujenzi wa kituo kipya cha ununuzi wa madini cha Lemshuku wilayani humo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuzitatua changamoto za maeneo hayo ili kuwa na miundo mbinu bora na salama.


"Natamani kuona Mirerani, Arusha, Geita, Chunya, Mara,Kahama na maeneo mengine nchini yanakuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito na metali Afrika. Nataka kuona Dubai ikihamia Simanjiro,” amesema Mavunde.


"Changamoto za maji, miundombinu, umeme, usalama vibali na huduma za kijamii katika maeneo ya uzalishaji huo zinafanyiwa kazi ili mnyororo wa thamani uendelee kuwajumuisha Watanzania na uchumi wa Tanzania kupitia sekta ya madini umilikiwe na Watanzania wenyewe". Amesema Mavunde.

Ujenzi huo umefikia asilimia 88 na Waziri amemwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mirerani kuongeza kasi ya ujenzi ili kituo kikamilike na kuanza kufanya kazi.


Maeneo ya Mirerani, Chunya na Kahama imekuwa kitovu cha ukuaji wa ajira kutokana na shughuli za uchimbaji madini ambazo zinahusisha zaidi vijana lakini shughuli hizo zimekuwa zikisababisha sintofahamu na migogoro hususani wachimbaji wadogo wanapokuwa hawajasajiliwa rasmi na serikali.


Hatua ya kutolewa kwa leseni hizo itachangia uwajibikaji kwa vikundi hivyo sambamba na kupata manufaa bila kuonekana kama walowezi.


Comments